Emeresiana Athanas
William Lukuvi |
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William
Lukuvi amesema asilimia 85 ya ardhi nchini haijapimwa, hali inayochangia watu
kuishi kwenye makazi holela.
Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa ufunguzi wa
Mkutano Mkuu na Kongamano la Wapimaji Ardhi uliofanyika jijini humo, Waziri
Lukuvi alisema Serikali inapoteza mapato kutokana na kuwa na sehemu kubwa ya
ardhi isiyopimwa.
Waziri huyo alitaka wataalamu hao kufanya kazi ili
kuepuka makazi hayo huku akibainisha kuwa wapimaji wa sekta binafsi wamekuwa
wakifanya vizuri kuliko walioajiriwa na Serikali.
Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwaagiza wataalamu hao
kupima ardhi ya viwanja 400 hadi mwishoni mwa mwaka huu.
Kuhusu masuala ya hati, Waziri Lukuvi alisema katika
miaka 10 ijayo ni lazima kila mtu awe na hati ya kiwanja au shamba lililopimwa.
"Ni lazima kuondokana na mfumo wa hati kwenye
karatasi na kuingia kwenye mfumo wa elektroniki katika kusaidia wananchi
wasidhulumiwe ardhi kwa kushirikiana na watumishi wasio waaminifu,"
alisema.
Waziri Lukuvi alisema ni marufuku kwa wapimaji ardhi
walioajiriwa na Serikali kuwa kampuni za upimaji ardhi ili kuondokana na
mgongano wa kimaslahi.
Rais wa Wataalamu hao, Martins Chodata alisema watashirikiana
na Serikali katika masuala ya upimaji ardhi pamoja na kufichua baadhi ya
wapimaji ardhi wasio na maadili na kusababisha migogoro.
0 comments:
Post a Comment