Maegesho ya magari Dar yapata wenyewe


Immaculate Ruzika

NAIBU Meya wa Jiji la Dar es Salaam Musa Kafana, ametangaza washindi wa zabuni ya kusimamia maegesho ya magari.

Hata hivyo ameitaja kampuni ya Kenya Airport kuwa licha ya kushinda, imejiondoa baada ya kukosa vigezo vinavyotakiwa kwenye mkataba wa kitabu cha tenda hiyo.

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam hivi karibuni, ilitangaza zabuni kwa wanaotaka kusimamia maegesho ya magari kwenye wilaya za Temeke, Ilala na Kinondoni.

Kutokana na tangazo hilo zilijitokeza kampuni za ndani na nje ya nchi huku kila moja akijinadi kuweza kukusanya mamilioni ya fedha kwa siku.

Kafana alitaja kampuni zingine zilizoshinda kuwa ni Epautwa iliyoshinda Temeke na Ubapa ya Kinondoni, huku Ilala ikiwa wazi baada ya Kenya Aiport iliyoshinda kwenye mchakato huo kukosa vigezo.

‘’Kenya Aiport ilishinda zabuni Ilala, lakini tumeshindwa kuingia nayo mkataba kwa kuwa haina vigezo vinavyotakiwa kwenye waraka wetu wa zabuni, hivyo tuliipa siku 28 kufanya marekebisho, lakini mpaka muda umepita haijawasilisha chochote,’’ alisema.

Meya huyo alitaja upungufu uliojitokeza kwenye kampuni hiyo kuwa ni pamoja na kukosa kibali cha kufanya kazi nchini, kukosa usajili wa BRELA, hivyo kukosa sifa.

Aidha Kafana alisema sasa makusanyo ya Ilala yanafanywa na kampuni ya NPS, ambayo imekuwa ikifanya kazi hiyo kwa muda mrefu

Ushindi wa kampuni hizo umekuja na kuiondoa kampuni ya Kinjeketile Parking System, iliyokuwa ikiendeshwa na Kinjeketile Ngombale-Mwiru ambaye ni mtoto wa mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo