Celina Mathew
Profesa Ibrahim Lipumba |
WAKATI wananchi wakilia kukaukiwa fedha
mifukoni, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ametaja baadhi ya mambo
yanayosababisha hali hiyo.
Profesa Lipumba ambaye kitaaluma ni
mchumi, alisema pamoja na jitihada zinazofanywa za Serikali kuhakikisha fedha
zinatumika vizuri ili kuondokana na matumizi ya hovyo, ipo haja kwa miradi yake
kutekelezwa kikamilifu.
Alisema Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT)
inaonesha hadi Julai, kwenye Bajeti fedha zilizokusanywa ni zaidi ya Sh trilioni
1.2 lakini matumizi ni Sh bilioni 800 jambo ambalo linaonesha makusanyo ni
mengi kuliko matumizi.
"Hali hiyo inaonesha kuwa Serikali
imechukua fedha nyingi kutoka kwa wananchi lakini kutokana na dhana ya kubana
matumizi, zimetumika kidogo sana jambo ambalo linafanya mzunguko wa fedha kuwa
mdogo," alisema.
Mchumi huyo alisema kwa kiasi kikubwa
hali hiyo imepunguza fedha kwa wananchi na mzunguko wake ndani ya uchumi
umepungua kwa kiasi kikubwa.
Profesa Lipumba alisema sababu nyingine
ni benki kutotoa mikopo kwa wakati na kasi, tofauti na ilivyokuwa awali hali inayosababisha
Serikali kukusanya mapato ya juu kuliko matumizi.
Aliongeza kuwa kwa kiasi kikubwa watu walitarajia
kuwapo semina, mikutano na vikao vya kawaida, jambo ambalo halijajitokeza hadi
sasa na hivyo kufanya fedha kutoonekana mitaani.
Hata hivyo, alisema athari zake kwa
ukuaji wa uchumi ni kuwa kwa robo ya pili ya mwaka iliyoishia Juni, haijulikani
robo ya tatu mambo yatakuwaje.
Pia, alisema mashirika ya umma kwa kiasi
kikubwa yamesitisha shughuli za ujenzi, hivyo kupunguza kasi ya kukua kwa
uchumi na mzunguko mdogo wa fedha.
Hivi karibuni, Rais John Magufuli
akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari alipingana na kauli kuwa uchumi
umeporomoka sambamba na fedha kukauka mifukoni mwa watu, kwa maelezo kuwa awali
watu walikuwa wakitambia fedha za dili, jambo ambalo kwa sasa halipo.
“Wakati wa kupiga dili kwa sasa haupo na
badala yake Watanzania wafanye kazi kwa bidii badala ya kukaa na kulalamika
bila sababu za msingi.
“Pia kwa kiasi kikubwa watu
wanaolalamika kuwa hakuna fedha kwenye mifuko ni wapiga dili na kama kuna mtu
ambaye anawaza fedha za dili hatazipata,” alisema.
0 comments:
Post a Comment