Enlesy Mbegalo
JIJI la Dar es Salaam linakabiliwa na
upungufu wa magari ya wagonjwa 38 ikiwa na magari 12 kati ya 50 yanayohitajika
hali inayochangia wananchi kukosa huduma stahiki.
Msimamizi wa Huduma za Dharura wa Mkoa
wa Dar es Salaam, Dk Christopher Mzava alisema hayo jana mbele ya waandishi wa habari kwenye semina ya
kuwajengeea uwezo madereva wa magari ya wagonjwa.
“Ukosefu wa magari hayo unasababisha ucheleweshwaji
wa wagonjwa kufika hospitali na kusababisha vifo. Angalau kila Halmashauri
ingekuwa na magari 10, kidogo yangepunguza changamoto iliyopo,” alisema Mzava.
Akifafanua, alisema Manispaa ya
Kinondoni ina vituo vya afya 40 lakini magari ni manne, Temeke vituo 42 magari
matatu na Ilala vituo 27 magari matano ambayo hayatoshelezi mahitaji ya huduma
hiyo.
Dk Mzava alitoa mwito kwa taasisi, mashirika
na watu binafsi kusaidia kuboresha kitengo hicho ili kitimize malengo yake kwa
kutoa huduma husika ili kuokoa maisha ya mama na watoto wachanga.
Inspekta wa Polisi kutoka Makao Makuu ya
Polisi, Yohana Mjema alisema madereva wa magari hayo na askari wa Kikosi cha
Usalama Barabarani, wanatakiwa kushirikiana ili kukabiliana na changamoto za
barabarani.
Dereva Ally Pingili alisema wanapokuwa
kwenye majukumu ya kazi zao, askari hao wamekuwa hawatoi ushirikiano kwao na
wakati mwingine wamekuwa wakiwajibu vibaya.
0 comments:
Post a Comment