Grace Gurisha
John Malya |
KESI ya kupinga matokeo ya umeya wa Kinondoni, ambayo
yalimpa ushindi Benjamin Sitta iliyofunguliwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) inatarajiwa kuanza kusikilizwa Novemba 16 na Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu, Dar es Salaam.
Hatua hiyo inakuja baada ya kesi hiyo kupangiwa hakimu
ambaye ni Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage.
Mbali na Sitta ambaye alipata kura zote 18 walalamikiwa
wengine katika kesi hiyo ni Naibu Meya, George Manyama (CCM), Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Kinondoni, Aron Kagurumjuli na Ofisa Tawala wa Manispaa hiyo.
Awali, Wakili wa Chadema, John Malya alisema walifikia
uamuzi wa kwenda mahakamani kutokana na mchezo mchafu uliochezwa na CCM kwenye
uchaguzi wa Meya Oktoba 23 ambao
uliambatana na ukiukwaji wa sheria na taratibu.
Malya alisema wanaiomba Mahakama itengue umeya wa Sitta
kwa sababu CCM walikaa mwenyewe na kujichagua, hali ambayo ilisababisha wao
wagomee uchaguzi huo.
"Tunaiomba Mahakama iamuru uchaguzi wa Meya ufanyike
kwa kufuata kanuni, isije kikatokea kama
kilichotokea awali kwa CCM kupanga matokeo," alisema Malya
Pia alisema katika hati yao, wanaiomba Mahakama iwaamuru
Kagurumjuli na wasimamizi wote wa uchaguzi wafuate taratibu za kisheria.
Aliongeza kuwa wanaiomba pia Mahakama iwaamuru wadaiwa
walipe gharama za kesi. Alisema walalamikaji katika kesi hiyo ni Diwani wa
Kinondoni, Mustafa Muro ambaye pia alikuwa mgombea umeya na aliyekuwa Naibu Meya,
Jumanne Mbunju.
Katibu wa Chadema wa Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kileo
alisema walikimbilia mahakamani kwa sababu haki yao iliporwa wazi wazi.
Alisema kilichosababisha uchaguzi wa Ubungo kuahirishwa
ni kukiukwa taratibu, hivyo Mkurugenzi
wa Ubungo na Ofisa Tawala wa Ubungo waliahirisha uchaguzi huo baada ya kubaini
taratibu zilikiukwa kama ilivyofanyika Kinondoni.
0 comments:
Post a Comment