*Mvutano wa Lipumba, Maalim wazuia
malipo
*Vitabu vya hundi vyafungiwa ofisini
Buguruni
Fidelis Butahe
SIKU 40 baada ya CUF kugawanyika mapande
mawili, wafanyakazi wa chama hicho wapatao 49 wanalia njaa baada ya kutolipwa posho
na fedha za kujikimu kuwawezesha kufanya shughuli mbalimbali kwa miezi mitatu.
Hali hiyo inatokana na wafanyakazi hao
kuwa sehemu ya mgogoro uliogawa chama
hicho; unaomwunga mkono Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu,
Maalim Seif Sharif Hamad, hivyo kuvuruga utaratibu wa malipo na matumizi ya
fedha.
Matumaini ya wafanyakazi hao kulipwa mishahara
yao ya Agosti, Septemba na Oktoba, yalianza kutoweka Septemba 23 baada
ya Profesa Lipumba na wafuasi wake, ‘kuvamia’ ofisi ya makao makuu ya chama
hicho Buguruni, ikiwa ni saa chache
baada ya kutambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, jambo ambalo liliwafanya wafuasi wa Maalim
Seif waliokuwa wakifanya kazi kuikimbia ofisi hiyo.
Habari kutoka ndani ya chama hicho,
zinaeleza kuwa njaa hiyo ilizaa harakati ya ‘usakaji fedha’, na ndicho chanzo
cha Maalim Seif kumbana Profesa Lipumba kwa kuandika barua kwa benki zote nchini
Oktoba 12, ili kudhibiti ruzuku ya chama isipite kwenye mikono ya kiongozi
huyo.
Hatua hiyo ilitokana na Msajili, Jaji
Francis Mutungi kumtambulisha Profesa Lipumba katika benki ya NMB tawi la Ilala
akitaka apewe ushirikiano wa kufungua akaunti mpya ya chama.
Hatua ya Profesa Lipumba kutaka kufungua
akaunti inatokana na barua ya Msajili Oktoba 6 iliyosainiwa na Naibu Msajili, Sisty
Nyahoza kwenda kwa Meneja wa benki hiyo.
Barua hiyo ni yenye kumbukumbu namba HA.
322/362/14/104 ambayo inamtambulisha Profesa Lipumba ili kufungua akaunti
mpya ya The Civic United Front (CUF).
“Siku Lipumba aliporejea, wafanyakazi
wengi walitaharuki na kukimbia ofisi. Wakaacha nyaraka zote muhimu vikiwamo
vitabu vya hundi za benki na mihuri yote muhimu,” alisema mmoja wa wafanyakazi
hao ambaye hakutaka kutajwa gazetini na kuendelea:
“Sasa kinachofanyika, hakuna fedha
inayoweza kutoka benki bila hundi kwa maana hiyo wafuasi wa Lipumba na Maalim
Seif wote wanalia njaa.”
Habari zaidi zilieleza kuwa awali
Profesa Lipumba alijaribu kulipa wafuasi wake kwa kutumia fedha zake za mfukoni
na alifanikiwa kufanya hivyo kwa mwezi mmoja tu, “baada ya hapo akashindwa
kuendelea na wote sasa tunalia njaa.”
Hali mbaya ya kifedha ndani ya chama hicho imetajwa
kuchangiwa zaidi na watia saini wa chama hicho kuidhinisha fedha benki kwa
ajili ya matumizi ya chama kutoka pande hizo mbili ambao ni Mbunge wa Kaliua,
Magdalena Sakaya (Kambi ya Lipumba) na Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi, Joram
Bashange aliyepo kwa Maalim.
Baada ya kutambuliwa na Ofisi ya
Msajili, Profesa Lipumba alitengua uteuzi wa wakurugenzi akiwamo Bashange huku
Sakaya akiwa amesimamishwa uanachama na Baraza la Uongozi la CUF, jambo ambalo
lilizua hali ya sintofahamu juu ya utoaji wa fedha benki.
Akizungumzia suala hilo, Kaimu Naibu
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma, Mbarara Maharagande alisema:
“Hakuna malalamiko yoyote, wafanyakazi waliopo katika utaratibu maalumu wa
chama (kambi ya Maalim Seif) wanalipwa.
“Kama kuna ambaye hajalipwa basi atakuwa
hayuko kwenye utaratibu sahihi wa chama. Wapo ambao walifukuzwa ndani ya chama,
hawawezi kuwa katika utaratibu wa malipo.”
Agosti 6 mwaka jana Profesa Lipumba
alitangaza kujiuzulu uenyekiti wa chama hicho na kueleza kukerwa na hatua za
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kushindwa kusimamia makubaliano yaliyozaa
umoja huo kuwakaribisha wanachama wa CCM na kupewa nafasi ya kuwania uongozi wa
nchi kupitia umoja huo.
Hata hivyo, Juni 8 mwaka huu, Profesa
aliandika barua ya kutengua uamuzi wake, jambo ambalo lilipingwa na wafuasi wa
Maalim Seif huku Mkutano Mkuu wa CUF ukiridhia barua yake ya kujiuzulu na
baadaye Baraza Kuu kumvua uanachama.
Hatua hizo zilizua mvutano wa kisheria
na Msajili Mutungi kulazimika kuingilia kati na kutoa ufafanuzi wa kisheria
huku akimtambua Lipumba kuwa Mwenyekiti, jambo ambalo linapingwa na kambi ya
pili.
0 comments:
Post a Comment