Leonce Zimbandu
MKUU wa Wilaya wa Kilosa mkoani Morogoro, Adamu Mgoyi
amesema hakuna taarifa ya kusitisha upigaji chapa wa mifugo, hivyo wilaya yake
inaendelea ikiwamo kusaka wafugaji wahalifu wanaoharibu mazao ya wakulima.
Wahalifu hao wanaendelea kusakwa na Kamati ya Usalama ya
Wilaya ili kuwachukulia hatua za kisheria na wakulima watumie fursa hiyo kuzalisha
chakula.
Mgoyi alisema hayo alipozungumza na gazeti hili jana kwa
njia ya simu ili kupata ufafanuzi wa sitofahamu ya mpango wa upigaji chapa
mifugo na uharibifu wa mazao.
Alisema
wafugaji jamii ya Kimasai wameachana na mgomo baridi na wanapeleka mifugo yao
kupigwa chapa baada ya kupewa elimu ya kutosha juu ya sheria inayosimamia kazi
hiyo na kuhakikishiwa usalama wa mifugo yao.
“Hadi Septemba
22 wilaya ya Kilosa imefanikiwa kupiga chapa ng'ombe 9,437 kati ya 140,110
waliotambuliwa katika kata za Berega, Mtumbatu, Mvumi, Magomeni, Dumila na
Mamboya,” alisema.
Awali mkazi
wa kijiji cha Tindiga, Salehe Juma alisema
ameshangazwa na taarifa kutoka kwa wafugaji kuwa mpango wa kupiga chapa mifugo
umesitishwa.
Alisema
iwapo mpango huo utasitishwa, mkakati wa upangaji matumizi bora ya ardhi katika wilaya hiyo,
hauwezi kufanikiwa.
“Tunamshukuru
Rais John Magufuli kufikiria na kutuletea Mkuu wa Wilaya Mgoyi ambaye ni
mwajibikaji na mfuatiliaji wa changamoto zinazokabili wananchi,” alisema.
Alisema
wanaomba Serikali iendelee kuwachukulia hatua wafugaji wahalifu ambao kwa
makusudi wanaharibu mazao ya wakulima.
0 comments:
Post a Comment