Suleiman Msuya
SHIRIKISHO la Vyuo vya Elimu ya Juu la CCM, limetoa siku
saba kwa Serikali na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB),
kuhakikisha wanatatua changamoto na malalamiko ya wanafunzi wanaohitaji mikopo.
Aidha, Shirikisho hilo limemwomba Rais John Magufuli ‘kutumbua’
watendaji wa Bodi hiyo kwa lilichodai kuwa ni kufanya hujuma dhidi ya Serikali.
Siku saba hizo zilitolewa jana na Katibu Msaidizi wa
Shirikisho hilo, Daniel Zenda wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es
Salaam huku hali ya sintofahamu kuhusu zaidi ya wanafunzi 27,053 kupata mikopo
ikiwa bado inaendelea.
Zenda alisema walilazimika kutoa siku hizo baada ya
kufanya utafiti na kujiridhisha kuwa wanafunzi waliokosa mikopo chanzo cha
tatizo ni Bodi hiyo kutotekeleza majukumu yake kwa ufasaha.
Alisema baada ya uchunguzi walibaini kuwapo utofauti
baina ya mwongozo wa Serikali na Bodi, jambo ambalo linawatia shaka.
Katibu Msaidizi huyo alisema wamegundua zaidi ya
wanafunzi 64 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na 78 wa Chuo cha
Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), wamenyimwa mikopo licha ya kuwa yatima na
kufaulu daraja la kwanza na pili.
Alisema MNMA ina wanafunzi 720 wenye sifa za kupewa
mikopo ila waliopewa ni 151 hali ambayo inaweza kusababisha wanafunzi kutoendelea
na masomo.
“Sisi ni wasomi wa chuo kikuu, tumefanya utafiti tumegundua
mambo ambayo yanafanywa na Bodi na tunaamini yana lengo la kumhujumu Rais
Magufuli, hivyo tunatoa siku saba changamoto za wanafunzi wa elimu ya juu ziwe
zimekwisha,” alisema.
Alisema Bodi hiyo ina kigezo cha kuwa mwenye umri wa zaidi
ya miaka 30 ananyimwa mkopo, jambo ambalo ni kinyume na haki za kupata elimu,
kwani kinachohitajika ni kuwa na ufaulu stahiki.
Zenda alisema Shirikisho linashauri mambo matatu, ambayo
ni Wizara husika na Bodi kuwa na vigezo vinavyofanana na shindanishi bila
ubaguzi kama uyatima, ulemavu, ufaulu na vingine.
Pili, alisema wanashauri ushirikishwaji wa wadau hasa
wanafunzi katika mchakato wa kuweka vigezo ili kuleta tija kwa jamii.
Katibu Msaidizi huyo alisema ushauri wa tatu ni
kuhakikisha upatikanaji wa mikopo unazingatia muda, ili kuepusha usumbufu kwa
wanafunzi.
Zenda alisema Shirikisho linapingana na mpango wa Bodi
kutaka kuhakiki na kuondoa wanufaika wa mikopo ambao wanafikiri kuwa hawatakuwa
na sifa na kwamba kufanya hivyo ni kuvunja sheria.
Aidha walitoa rai kwa Serikali kupitia Ofisi ya Mkaguzi
na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukagua fedha zaidi ya Sh bilioni
1.7 zinazotokana na ada za kuomba mikopo kwa mwaka huu ili kujua matumizi ya
fedha hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul Razaq Badru alisema wanafunzi 25,717 wa
mwaka wa kwanza ndio watapata mikopo kwa mwaka 2016/17 kati ya 58,000 ambao
waliwasilishwa na Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU) kwa Bodi hiyo.
Badru alibainisha mgawanyo wa mikopo hiyo kuwa ni yatima
4,321, walemavu 118, waliofadhiliwa na taasisi 295, wanaosoma kozi za
vipaumbele 6,159 na wanaotoka familia duni 9,498.
0 comments:
Post a Comment