Suleiman Msuya
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa
Ibrahim Lipumba na wafuasi wanaomuunga mkono, wanasubiri hatua ya Katibu Mkuu
wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad na wafuasi wake kwenda mahakamani
kuzuia utekelezaji wa maelekezo ya msajili wa vyama mahakamani.
Uamuzi huo umekuja wakati upande wa
Maalim Seif ukieleza kuwa katika maandalizi ya mwisho ya kuwasilisha mahakamani
maombi ya kutoa zuio la barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambayo ilimtambua
Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti wa halali wa chama hicho.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi CUF,
anayetajwa kuwa upande wa Lipumba, Abdul Kambaya alisema wanachosubiri ni
maelekezo ya mahakama kama kweli Seif ataenda kortini.
“Sisi hatuna cha kufanya, tunasubiri
Seif na wenzake waende mahakamani. Nadhani uamuzi wa mahakama ndiyo utatoa
mwongozo wa sisi kuchukua hatua au kukaa kimya,” alisema Kambaya.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya
CUF upande wa Maalim Seif, Julius Mtatiro aliliambia JAMBO LEO kwamba baada ya
Mahakama Kuu kukubali na kuwaruhusu kuwasilisha ombi lao, mawakili wao wapo
katika hatua za mwisho kuwasilisha shauri hilo mahakamani.
“Kwa sasa tupo katika maandalizi ya
kuwasilisha Mahakamani kuhusu ombi letu la kutoa zuio la msajili kwani hakutendea
haki chama,” alisema.
Aidha, alisema CUF wanapeleka ombi
lingine mahakamani ambalo litatoa onyo kwa Msajili kuingilia uamuzi wa vyama vya
siasa kwani anavunja sheria na Katiba.
Mtatiro alisema Msajili ameonesha
dhahiri kwamba anatumikia kundi mojawapo katika mgogoro wa chama hicho, jambo alilosema
halikubaliki katika mfumo wa vyama vingi.
Katika hatua nyingine, Kambaya alisema
Lipumba anatarajiwa kuanza ziara nyingine mikoani mwishoni mwa mwezi huu hiyo
ikiwa ni baada ya kurejesha kutoka mikoa ya Kanda ya Kusini.
0 comments:
Post a Comment