SMZ: Marubani watatangaza utalii Zanzibar


Mary Mtuka, Zanzibar

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema kufika kwa marubani 22 ambao wako kwenye msafara wa ndege za zamani zilizotengenezwa mwaka 1920 na 1930 utakuwa chachu ya kutangazwa kwa utalii wa visiwa hivyo.

Hayo yalisemwa juzi na Mkurugenzi wa Masoko na Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Dk Miraji Ukuti Ussi, wakati wa mapokezi ya msafara wa ndege hizo ambazo ziliwasili visiwani hapa mchana zikitokea Arusha.

Alisema Zanzibar inajisikia fahari kupokea marubani wa ndege hizo na kueleza wazi kuwa wanaamini itakuwa chachu ya utalii wa Zanzibar kwani wengi wanaufuatilia msafara huo.

"Msafara wa ndege hizo unafahamika kwa jina la Vintage Air Rally na Wazanzibari wengi wamepata nafasi ya kujifunza kwa vitendo kwa kuona namna ambavyo ndege zilivyokuwa miaka ya zamani.

"Pia ujio wa ndege hizo unafungua fursa ya kutangaza utalii wetu. Kote ambako msafara huo umepita nchi mbalimbali duniani zimekuwa zikipata taarifa kupitia vyombo vya habari.

"Na hivyo marubani hao nao watakuwa sehemu ya kuueleza uzuri wa Zanzibar watakaporudi kwenye nchi zao," alisema.

Ussi alisema Zanzibar inatamani kuona inakuwa mwenyeji wa kuandaa msafara wa ndege hizo, kwani uwezo huo wanao na wanaamini hiyo itakuwa nafasi nyingine ya kuileza dunia kuwa uzuri wa Tanzania na maeneo yake ya utalii.

Pia alisema kitendo cha ujio wa ndege hizo kisiwani hapa kitachangia ongezeko la watalii visiwani na Tanzania kwa jumla kutokana na marubani wake kwenda kutembelea sehemu za utalii.

"Tunaamini  kuja kwao nchini watakuwa mabalozi wazuri wanaporejea nyumbani kwao watakwenda kuitangaza Zanzibar kwa kile watakachokiona, kwani tuna kila sababu ya kwamba mgeni afurahie kuanzia huduma na anachohitaji," alisema.

Aliongeza kuwa ndege hizo kutua Zanzibar ni kuutangaza utalii kwani msafara huo unafuatiliwa na mataifa duniani na hivyo utalii wa Zanzibar nao utafahamika zaidi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Puma Energy Tanzania Ltd,  Philippe Corsaletti alisema ujio wa ndege hizo ni nafasi nyingine ya kuutangaza utalii wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

"Msafara huo ambao ratiba yake inaonesha unapita kwenye nchi 10 ikiwamo Tanzania, umefungua milango ya utalii, kwani marubani   watakuwa mabalozi wazuri wa kutangaza utalii wetu," alisema.

Alisema msafara huo unatamgaza utalii wa Tanzania kwa kupita kwenye vivutio nchini na kabla ya kuwasili Zanzibar marubani hao walipita Ngorongoro, Serengeti na kujionea Mlima Kilimanjaro.

"Kabla ya kuondoka Arusha ndege hizo zilijazwa mafuta aina ya Avigas yaliyotolewa na wadhamini, Puma," alisema.


Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo