Wananchi waomba elimu ya hisa


Abraham Ntambara

WAKATI Serikali ikizitaka Taasisi zenye leseni za mawasiliano nchini zikiwamo kampuni za simu kuhakikisha zinawekeza asilimia 25 ya hisa zao kwa Watanzania kabla ya keshokutwa kwa kuzingatia sheria ya soko la hisa na dhamana, wakazi wa Dar es Salaam wamesema hawana uelewa mzuri wa masuala ya hisa.

Hivyo wameiomba Serikali kuendesha kampeni maalumu ya kuwaelimisha juu ya suala hilo na namna watakavyozinunua.

Wakizungumza na JAMBO LEO jana kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi hao walisema Serikali ina nia njema kwa wananchi wake lakini inatakiwa elimu ya ufahamu wa hisa.

Ally Said alisema kuna uelewa mdogo miongoni mwa wananchi juu ya suala la hisa akieleza kuwa mtu anapoelezwa kitu cha namna hiyo ni vigumu kuelewa.

“Serikali ina nia nzuri, lakini inatakiwa kazi ya zaida katika kuelimisha wananchi,” alisema Said.

Philemon Mfugalo alibainisha kwamba kunahitajika semina zitakazoelezea kwa undani kuhusu hisa ili kuamsha wananchi na kujua jinsi watakavyopata asilimia hizo kwa kuzinunua na kujua watakavyonufaika.

Aidha, aliongeza kuwa kutokana na uelewa mdogo, baadhi ya wananchi watashindwa kununua hisa hizo kwa kuhofia kuwa wanaweza kuibiwa.

“Suala hili ni zuri kiuchumi kwa mwananchi, ila inatakiwa wataalamu wa masuala ya uchumi kwa kushirikiana na Serikali wafanye kampeni maalumu kuufahamisha umma juu ya hilo,” alisema Mfugalo.

Hawa Rajabu alisema hana taarifa za Serikali kuzitaka kampuni za mawasiliano kuuza asilimia 25 ya hisa kwa wananchi na kubainisha kuwa zilikuwa ngeni kwake.

Pia alieleza kutolewa chochote kuhusu hisa akisema kutokana na hali hiyo hawezi kuzungumza lolote kuhusu hisa.

“Sina uelewa wowote, kwa hiyo siwezi kuongea lolote kuhusu hisa,” alisema Rajabu.

Akizungumza juzi na waandishi wa habari Dar es Salaam, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alizitaka kampuni zote ambazo leseni zao zilitolewa kabla ya Julai mosi kuuza hisa hizo kwa wananchi na kujisajili kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kwa kipindi kisichozidi miezi sita tangu kuanza kwa kipindi hicho.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo