Mpigapicha Mpoki Bukuku afariki dunia

Salha Mohamed

Mpoki Bukuku
MPIGAPICHA mwandamizi wa kampuni ya The Guardian Limited, Mpoki Bukuku (44), amefariki dunia.

Bukuku alikumbwa na mauti jana asubuhi kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kupata ajali juzi usiku Mwenge, Dar es Salaam.

Taarifa za ajali ya Bukuku zilianza kusambaa jana asubuhi, zikieleza kuwa alivunjika miguu na mkono wa kushoto katika ajali hiyo ya kugongwa na gari akitembea kwa miguu na kiukimbizwa Muhimbili.

Akizungumza na gazeti hili jana kwa simu, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma, Taasisi ya Tiba ya Mifupa ya Fahamu (MoI), Almas Jumaa, alisema Bukuku aliaga dunia saa nne asubuhi jana wakati madaktari wakimhudumia.

“Tulimpokea Bukuku kutoka MNH, leo (jana) saa 11 alfajiri baada ya kupata ajali ya gari iliyosababisha kuumia akivunjika baadhi ya viungo vyake,” alisema.

Alisema wakati wanampokea, majeruhi alionekana na maumivu upande wa kushoto wa mwili na madaktari walibaini ndiko alikoangukia.

Almasi alisema Bukuku alivunjika mbavu tatu za kushoto, miguu na mkono wa kushoto.

“Alikuwa na michubuko mwilini hasa kichwani, lakini alionekana na majeraha kwa ndani ya mwili,” alisema Almas.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Guardian Limited, Richard Mgamba katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, alielezea namna alivyopokea taarifa za msiba huo.

“Kama ilivyo kwa wengine wengi, nilipokea kwa mshituko mkubwa na kutoamini kifo cha ghafla cha mmoja wa wapigapicha waandamizi wa The Guardian Limited, Mpoki Bukuku, aliyefariki dunia Muhimbili.

“Kwa familia yake, wamepoteza baba, mume na zaidi ya yote rafiki wa kweli, lakini kwetu sisi The Guardian Limited, tumepoteza pia rafiki wa kweli na nguzo katika tasnia ya uandishi wa habari,” alisema Mgamba.

Mgamba alisema Bukuku alikuwa mwanadamu tu kama ilivyo kwa yeyote, lakini katika uandishi wa habari, aliipenda fani yake na hakuogopa kupambana ilimradi apate habari nzuri.

Alifafanua kuwa ujasiri wa Bukuku uliosababishwa na kiu yake ya kupata habari nzuri kuliko wengine, wakati mwingine ilimweka matatani.

Kupigwa

“Wale wanaoelewa uandishi wa habari wa picha, watabaini kwamba ujasiri na kuipenda kazi ni sifa kuu mbili za kila mpigapicha, ili apate habari nzuri na yenye nguvu. Bukuku alikuwa na sifa zote hizo. Alikuwa shujaa na mwenye mapenzi na kazi yake, hasa wakati akifuatilia habari kubwa kokote nchini.

“Alipigwa na hata kuteswa na maadui wa uhuru wa vyombo vya habari, lakini bado mahaba yake katika kufanikisha habari bora hayakuzimwa. Alikuwa mwandishi wa habari si kwa bahati mbaya, bali kwa kuchagua na ndiyo maana alikuwa na mapenzi wakati akitimiza wajibu wake wa kutekeleza kazi za kihabari alizopangiwa na wahariri wake,” alisema na kuongeza:

“Bukuku amemaliza safari yake duniani, kimwili hayuko nasi lakini kiroho na kiweledi, mara zote atakuwa nasi daima. Sisi katika The Guardian Limited tunaungana na familia, ndugu na marafiki katika kipindi hiki kigumu, kuomboleza msiba wa mtu ambaye tumekuwa tukifanya naye kazi kwa miaka mingi.”

Mgamba aliongeza kuwa kampuni hiyo itaunga mkono kwa ukamilifu familia ya marehemu Bukuku, ambapo kwa niaba ya wafanyakazi wa The Guardian Limited, alitoa salamu za rambirambi kwa mjane wa Bukuku, Lucy, watoto na wadau wote wa tasnia ya habari nchini, kwa kifo cha ghafla na cha kushitua cha mmoja weo.

Waziri

Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, alituma salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa wapiga picha pamoja na wanahabari wote nchini, kwa kifo cha Bukuku.

Taarifa ya Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari, ilieleza kuwa Nape pamoja na watendaji wa Wizara walipokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha mwanahabari huyo, kwani ni pigo kwa tasnia ya habari nchini.

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha mwanahabari Mpoki Bukuku. Kifo chake ni pigo kwa tasnia ya habari hususan katika picha , nimehuzunishwa sana kwa sababu marehemu wakati wa uhai wake, alitoa mchango mkubwa kwenye vyombo vya habari yakiwamo magazeti ya Majira, Business Times , The Guardian , Nipashe, Mwananchi na The Citizen,” alisema Nape katika taarifa hiyo na kuongeza:

“Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi. Amina.”

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo