ORODHA YA VYAKULA VISIVYO SALAMA


WANASAYANSI wanaamini karibu kila mtu ana matatizo yasiyopungua matatu ya kiafya ambayo ama yamekuwa sugu au anayachukulia tu kama sehemu ya maisha yake kwa sababu haelewi tiba.

Badala ya kukaa na matatizo, gazeti hili linakupa nafasi ya kueleza kero zako ili ujibiwe na watalamu mbalimbali wa afya.

Yafuatayo ni majibu ya baadhi ya wasomoja wa JAMBO LEO.

Swali: Dokta naomba unipe orodha angalau fupi ya vyakula hatari kwa afya ya binadamu

Jibu: Vyakula vinavyoweza kuleta madhara kwa binadamu ni vyote ambavyo havishauriwi au vimepigwa marufuku na wadhibiti wa vyakula kama vile TFDA.

Ninashauri ujifunze jinsi ya kula vyakula vyenye virutubisho sahihi (balanced diet), ambavyo ni wanga, mafuta, protini, madini, vitamini na maji. Vyakula hivi vyote lazima vitumiwe katika kiwango kinachohitajika.

Lakini pia tafiti zinataja baadhi ya vyakula ambavyo vikitumi  wa bila uangalifu vinaweza kuleta madhara katika mwili wa binadamu. Baadhi ya vyakula hivi ni:

• Vyakula vyenye mafuta mengi
• Vyakula vya kukaanga mafano chips)
• Vyakula vyenye chumvi au sukari nyingi.

vile kisukari, kansa, shinikizo la damu na uzito wa kupindukia

Ni vizuri pia kumtembelea mtaalamu wa mambo ya vyakula (Nutritionist) kwa msaada zaidi, na pia usikose kusoma makala zijazo katika gazeti hili ili kupata maelezo zaidi.

Swali: Nimetumia dawa za phenobabiton kwa muda wa miaka 30. Je zinaweza kuniathiri kiafya?

Jibu: Pole sana kwa tatizo ulilonalo. Swali lako halikueleza kwa nini unatumia dawa aina ya Phenobarbital, lakini dawa hii yaweza kutumika aidha kwa muda mfupi au muda mrefu kulingana na aina ya tatizo ulilo nalo. Kama zilivyo dawa nyingine, Phenobarital pia ina madhara yake inapotumika bila maelekezo maalum ya daktari. Ninakushauri urudi kwa daktari aliyekuandikia dawa hii, au daktari mwingine yeyote mwenye uelewa wa tatizo lako, ili muweze kuona kama bado unaihitaji au hapana, na kama dalili zote zilizokufanya uanze kutumia dawa hii zimekwisha au bado zipo. Kiujumla dawa hii ina madhara ya aina mbili, madhara ya muda mfupi au yale ya muda mrefu. Madhara ya muda mfupi ni:

• Kizunguzungu, kujisikia kusinzia kila wakati, maumivu ya kichwa, uchovu, kupoteza hamu ya kula, kichefuchefu na kutapika.

Madhara ya muda mrefu mengi ni yale yanayohusiana na mfumo wa fahamu kama:

• Mabadiliko ya tabia (mfano kuwa na hasira za haraka) na msomgo wa mawazo.

Matatizo mengine yanayoweza kutokea ni madhara ya ngozi, madhara ya mfumo wa damu, na mifumo mingi ya mwilini.

Pamoja na madhara niliyoyataja hapo juu, ikumbukwe kuwa si kila mgonjwa anayetumia dawa hizi ni lazima apate madhara haya. Dawa hii ni kama dawa nyingine na inapotumika kwa nia iliyokusudiwa husaidia kutibu tatizo kusudiwa.

Swali: Naitwa Albert. Naomba kuuliza endapo mtu utokunywa chai je,unaweza kupata tatizo gani?

Jibu: Ndugu Albert, kama nimelielewa vizuri swali lako vizuri, kutokunywa chai hakuwezi kukusababishia tatizo lolote. Unaweza kutafuta mbadala kwa kunywa viburudisho vingine zaidi ya chai kama juisi, maji, maziwa na vinginenyo.

Swali: Naitwa Justin nipo Kagera, swali langu ni kwamba mgonjwa akiwa anafanyiwa operesheni huwa anaumia sana na je ni mbinu gani mnatumia kuziba ngozi iliyopasuliwa?

Jibu: Ndugu Justin, hongera sana kwa kuwa na ndoto ya kuwa daktari bingwa wa magonjwa ya watoto (Paediatrician), jitahidi kusoma sana na ndoto zako zitatimia siku moja. Mgonjwa anapofanyiwa upasuaji huwa haumii kwa sababu hupewa dawa za kuzuia maumivu au hata za kumfanya alale usingizi kama anafanyiwa upasuaji mkubwa.

Njia inayotumika kuziba ngozi iliyofanyiwa upasuaji ni kwa kuishona kwa aina fulani ya nyuzi (surigal sutures) au kwa kutumia pini maalum (staples) na kusubiri jeraha lipone kwa wakati.

Swali: Mimi ni mjamzito, nina mimba ya miezi minne lakini nasumbuliwa na typhoid (Homa ya matumbo).

Nimetumia dawa nyingi lakini hali bado. Sasa nataka kujaribu matibabu kwa mtu mmoja anayetibu kwa miti shamba. Je haitaleta madhara?

Jibu: Pole sana mama. Sijajua ni dalili gani ulizonazo na ni kipimo gani umetumia kupima tatizo lako. Ni vizuri kuwa mwangalifu kwa sababu baadhi ya vipimo vya ugonjwa wa homa ya matumbo (typhoid fever) vinaweza kuonesha kwamba una tatizo hilo hata baada ya miezi kadhaa baada ya kutibiwa.

Wakati wa ujauzito tunashauri dawa yoyote unayokunywa ni lazima iwe imeshauriwa na mtaalamu wa afya ili isilete madhara katika ujauzito wako.

Kwa kifupi baadhi ya dalili za ugonjwa wa typhoid ni joto la mwili kuongezeka kadiri siku zinavyokwenda, maumivu ya kichwa, maumivu ya tumbo, kuharisha au kufunga choo, kutoka jasho jingi, kukosa hamu ya kula na tumbo kujaa gesi.

Hivyo basi, kabla ya kufanya maamuzi yoyote yale, ambayo yanaweza kuhatarisha afya yako na ya mwanao anayetegemea kuzaliwa hivi punde, ni lazima kuzingatia yote niliyoeleza hapo juu.

Swali: Naomba ushauri umri ni zaidi ya miaka 50  usingizi kwangu sipati kabisa nifanye nini? Ninaweza kukaa siku mbili sipati kabisa usingizi. Nikiingia kitandani ninakuwa kama nasubiri kuche. Mara chache naweza kusikia kama nasinzia lakini nikifika kitandani, usingizi unaisha. Nituumie nini ili niwe napata usingizi?

Jibu: Pole sana ndugu. Kukosa usingi ni tatizo ambalo linahitaji uchunguzi wa kina. Daktari anatakiwa kukuona na kuchukua historia yako kwa kirefu ili kuweza kubaini tatizo.

Endapo chanzo cha tatizo lako la kukosa usingizi (Insomnia) hakitatatuliwa, kuna hatari ya kuendelea kukosa usingizi na hatimaye kupata madhara mengine zaidi. Tafiti mbali mbali zinataja baadhi ya sababu zinazoweza kusababisha ukosefu wa usingizi kuwa magonjwa kama depression, msongo wa mawazo, mabadiliko ya mazingira na ratiba za siku, baadhi ya madawa kama nicotine (inapatikana kwenye sigara) na caffeine (inapatikana kwenye kahawa na chai ya rangi).

Sababu nyingine ni ulevi na baadhi ya magonjwa ya akili. Hivyo unatakiwa kumuona mtaalamu wa afya li aweze kujua kama unahitaji kupewa dawa au kupewa ushauri na matibabu mengine zaidi.

Swali: Naitwa Baraka, nipo Tabora nina tatizo la kukojoa mkojo wa njano unatoka wa moto sana halafu kwa ndani kunawasha, natamani kujikuna muda wote. Je nitumie dawa gani ili niweze kupona tatizo hilo?

Jibu: Pole sana Baraka. Kutokana na dalili ulizozitaja inaonekana una tatizo la maambukizi ya bakteria ya njia ya mkojo au kwa lugha ya kitaalamu ni UTI.

Dalili nyiningine za UTI ni kama kukojoa mara kwa mara, maumivu chini ya tumbo, homa kali, kujisikia mkojo umejaa kwenye kibofu ili hali ukienda kukojoa hupati mkojo kwa kiasi ulichotegemea.

Ninakushauri uende hospitali ya karibu ili umpe daktari historia kamili ya matatizo yako na yeye atakufanyia vipimo sahihi vikiwemo vya mkojo, na kukutibu tatizo lako. Pia nakushauri unywe maji kwa wingi, hii itakusaidia kubadili rangi ya mkojo wako kuwa ya kawaida.

Swali: Mimi ni msichana wa miaka 26, tatizo langu kila siku tumbo langu linakuwa kubwa kuzidi ujauzito wenye muda wa kujifungua. Je nifanyeje. Maana kila nikienda hospitali kupimwa sikutwi na tatizo ambalo linaweza kuwa chanzo cha tumbo langu kuwa kubwa. Anna,Temeke Dar es salaam.

Jibu: Pole sana Anna. Sababu za tumbo kuwa kubwa zipo nyingi, ni vigumu kuzitaja zote katika nafasi hii ndogo. Pia ingekua rahisi kwangu kama ningejua ulipoenda hospitali ni vipimo gani ulifanyiwa.

Ninakushauri urudi hospitali na uombe kuonana na daktari bingwa (Physician). Kama hapatikani katika hospitali yako, basi waweza kuomba rufaa ili uende kwenye hospitali kubwa zaidi kwa ajili ya kumuona daktari bingwa na kufanyiwa vipimo na matibabu zaidi.

Swali: Naomba kujua tumbo la chakula kwa kawaida linatakiwa lipate chakula chenye kipimo cha uzito gani kwa mlo?

Jibu: Kwa kawaida kiasi cha chakula unachotakiwa kula hakipimwi kwa mzani fulani. Kinachotakiwa kufahamika ni kipimo gani cha nguvu (energy) mtu anatakiwa apate kwa siku.

Kipimo hiki huitwa kalori (calorie), na mwanaume wa kawaida mwenye uzito wa wastani anahitaji angalau chakula chenye kalori 2500 (2500 calories) kwa siku, wakati mwanamke mwenye uzito wa wastani anahitaji angalau kalori 2000 (2000 calories) kwa siku.

Swali: Natamani kujua tiba ya fangas sehemu za siri. Nawashwa ukeni. Haja ndogo naumia. Nikifanya tendo la ndoa navimba. Mara kwa mara natokwa na uchafu ukeni. Ni uchafu mweupe na wakati mwingine una rangi ya njano. Je sababu ni nini? Ni ugonjwa gani?

Jibu: Pole sana ndugu. Kwa dalili ulizozitaja kwenye swali lako inaoneka una maambukizi ya fangasi aina ya candida za ukeni.

Fangasi za ukeni husababishwa na mabadiliko ya hali ya asidi ambayo ndiyo inayotakiwa kuwepo ukeni, badala yake hali ya alikali (Alkaline) huongezeka, hii husababisha kupungua kwa baadhi ya bakteria wenye faida ambao ndio huzuia kusambaa kwa candida. Tatizo la fangasi za ukeni pia hutokea mara kwa mara kwa akina mama wajawazito na wale wasio wajawazito hasa wakati wa hedhi. Ninakushauri uende hospitali kwa vipimo na matibabu kwa sababu tatizo hili linatibika.

Swali: Naitwa Rajab Kaila. Ni dereva. Huwa napata tabu usiku nikiwa naendesha lori. Nasumbuliwa na usingizi sasa. Naomba ushauri nini cha kufanya ili nisipate usingizi wakati wa usiku nikiwa naendesha.

Jibu: Ndugu Rajab, kwa kawaida inapofika usiku ubongo na mwili kwa ujumla vinahitaji kupumzika. Ninakushauri ni vizuri ukau-tumia usiku kupumzika kiasi cha kutosha na mchana kuendelea na safari yako.

Kama ni muhimu sana kusafiri usiku kutokana na aina ya kazi yako, basi ninakushauri upate muda wa kutosha wa kulala nyakati za mchana. Binadamu anahitaji angalau masaa saba mpaka nane ya kulala kila siku.

Kutokuzingatia hili, kunaweza kukupelekea kupata madhara mengine ya kiafya na hata uwezekano wa kupata ajali barabarani.

Maoni au maswali tuma kwa simu 0713247889 au kwa baruapepe: afya@jamboleo.net

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo