Seif ajibu hoja za Jaji Mutungi


Enlesy Mbegalo

CHAMA cha Wananchi (CUF), kimemjibu Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kikisema ofisi yake haina mamlaka ya kisheria kutoa msimamo na mwongozo wa chama kilichosajiliwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Hamad, majukumu ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliyoanzishwa kwa Sheria ya Vyama vya Siasa sura 258 haimpi Jaji Mutungi mamlaka hayo.

Alisema sheria hiyo inampa mamlaka ya kuhifadhi kumbukumbu na taarifa za vyama vya siasa na siyo kuviamria vyama.

“Baraza Kuu la Uongozi wa CUF linasikitika na upotoshaji wako wa makusudi ulioufanywa na ofisi yako kuhusu tafsiri ya vifungu vya Sheria ya Vyama Vya Siasa, Sura ya 258 ulivyovitaja katika ukurasa wa pili wa taarifa yako fupi ili kujipa mamlaka ya kushughulikia kile ulichokiita mgogoro wa uongozi katika chama chetu,” alisema.

Alisema hakuna chama cha siasa kitakachofaulu kupewa usajili wa kudumu hadi kiwe kimewasilishwa majina ya uongozi wa kitaifa na uongozi wa chama hicho uundwe na wanachama kutoka Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara.

Alisema ukisoma vifungu hivyo katika sheria hiyo utabaini kuwa hakuna uhusiano na kukupa mamlaka au wajibu wa kuchunguza na kujiridhisha kuhusu usahihi wa mabadiliko katika uongozi wa kitaifa wa chama na ama kutengua au kubariki uamuzi halali wa vikao halali vya chama chochote.

Aliongeza kuwa kwa kujiuzulu kwa Profesa Ibrahim Lipumba na kutengua barua yake Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF linatambua kuwa chama cha hicho kinaongozwa na Katiba yake halali, toleo la mwaka 2014.

“Tunapenda utambue (Msajili) kuwa kujiuzulu kwa kiongozi ni wakati wowote kwa mujibu wa Ibara ya 117(1). Kuhusu utaratibu uliowekwa na ibara ya 117(2) hauathiri haki ya kiongozi kujiuzulu wakati wowote,” alisema Maalim Seif. Alisema Profesa Lipumba aliandika barua ya kujiuzulu nafasi ya Mwenyekiti wa CUF Taifa kuanzia tarehe 5/08/2015.

Alisema Lipumba alijiuzulu rasmi nafasi yake ya uenyekiti wa Taifa CUF Agosti 5 mwaka jana huku akidai kuendelea kuwa mwanachama na kadi yake aliilipia mpaka 2020 hivyo alitekeleza kujiuzulu kwake bila kusubiri kukubaliwa na Mkutano Mkuu wa Chama kwa mujibu wa Ibara 117(2) ya Katiba ya CUF.

Aliongeza kuwa Lipumba alikuwa na mamlaka ya kuhakikisha Mkutano Mkuu unaitishwa ili kukubali kujiuzulu kwake, lakini hakufanya hivyo.

“Kama ulivyoeleza katika taarifa yako, Katiba ya CUF inatambua haki ya kujiuzulu uongozi lakini haizungumzii kutengua uamuzi wa kujiuzulu,” alisema. Maalim Seif alisema Profesa Lipumba asingeweza kutengua uamuzi wake wa kujiuzulu kwa sababu alishautekeleza.

Alisema suala la Profesa Lipumba kurudi kwenye nafasi ya Mwenyekiti wa CUF Taifa baada ya zaidi ya miezi kumi ni wazo chelewefu na ndiyo maana amekuwa akiitika wito wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kama mwaliko kutoa maoni juu ya mambo mbalimbali.

“Tambua pia kuwa Katiba ya CUF ni yetu wenyewe na wewe ni Msajili, tunaifahamu vyema sisi wanachama na viongozi kuhusu maudhui yake kuliko wewe ambaye mara zote tunakupa taarifa baada ya maamuzi ya vikao na Katiba hiyo kuwasilishwa kwako kwa usajili tu,” alisema. Alisema kujiuzulu kwa Lipumba kulifanyiwa maamuzi kwa mujibu wa Ibara ya 115(1) ya Katiba ya CUF na siyo ibara ya 77(7).
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo