Serikali yataka wakeketaji wakamatwe


Leonce Zimbandu

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imevitaka vyombo vya Dola  kukamata wazazi, walezi, mangariba na wanaoendeleza vitendo vya ukeketaji dhidi ya watoto wa kike na wasichana katika kata ya Kivule na maeneo mengine nchini.

Agizo hilo lilitolewa jana kutokana na taarifa ya ukeketaji hivi karibuni kwenye kata ya Kivule, Ilala, Dar es Salaam na mikoa mengine ambayo ilikaririwa na vyombo vya habari. 

Msemaji wa Wizara hiyo, Erasto Ching’oro alisema hayo alipozungumza na gazeti hili Dar es Salaam.

Alisema  athari za ukeketaji ni majeraha kwa watoto, vifo, vilema, maradhi, ikiwamo fistula na mengineyo.

Aliendelea kusema kuwa watoto wa kike na wanawake wamekuwa wakifanyiwa ukatili huo bila ridhaa yao na wakati mwingine ridhaa hupatikana kwa hila, jambo ambalo ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

Wizara tunaendelea kupambana na ukeketaji  na kuongeza juhudi ya utoaji elimu kwa jamii ili kuwachukulia hatua wanaojihusisha na mila hiyo potofu,” alisema.

Alisema wananchi wanapaswa kushiriki kuzuia vitendo vya ukeketaji na hasa kufichua ukeketaji na kutoa ushahidi mahakamani ili wahusika wachukuliwe hatua.

Aidha, Wizara ilitoa rai kwa maofisa maendeleo ya jamii na maofisa ustawi wa jamii wa mikoa, halmashauri na kata  kuzuia ukeketaji kwa kushirikiana na mamlaka husika.

Alisema wazazi na walezi wanatakiwa kuacha ukeketaji kwa kuwa  ni ukatili kwa watoto wa kike na kosa la jinai, vinginevyo  watafikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo