Ofisi ya AG yakana barua mtandaoni


Sharifa Marira

Asiatu Msuya
NAIBU Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Asiatu Msuya, amesema taarifa zilizoenea kwenye mitandao ya kijamii kwamba ofisi hiyo imepiga marufuku watumishi wake kupewa mikopo na taasisi za fedha nchini mpaka ithibitike kuwa hawadaiwi mikopo ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), si za kweli.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi hiyo jana, haina mamlaka ya kuzuia wala kuruhusu mtumishi kukopa kwenye taasisi yoyote ya fedha.

"Ikumbukwe kuwa mikopo yote ya watumishi wa umma kwenye taasisi za fedha, hutolewa kwa kuzingatia sharia, kanuni na taratibu zilizopo, ilimradi mtumishi awe na vigezo,” alisema Msuya.

Aliwataka watumishi wa umma kutojihusisha na usambazaji taarifa za uongo na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angella Kairuki alipoulizwa na mwandishi wetu kuhusu uwepo wa taarifa hizo, alisema: ‘’Hilo ni agizo la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali lililotolewa kwa wafanyakazi wake, ikiwa ni sehemu ya utaratibu wao wa kazi.’’

Alipoulizwa kama ni tamko linalopaswa kutekelezwa kwa watumishi wote wa umma, alisema Ofisi ya AG ndiyo yenye jukumu la kuzungumzia suala hilo kwa kuwa tangazo limetoka ofisi yake.

‘’Unazungumzia tangazo lililo kwenye mitandao ya kijamii, ni kweli nimeliona, lakini limetolewa na Ofisi ya AG ambaye  leo (jana) alikuwa anazungumza na waandishi wa habari kuhusu suala hilo hilo, sasa nadhani ingekuwa vizuri mkawasiliana naye, sipaswi kuwazungumzia,’’ alisema Kairuki.

Taarifa iliyosambaa kwenye mitandao ilielekezwa kwa wakurugenzi wa divisheni, wakuu wa vitengo, mawakili wa serikali wafawidhi, mikoa na wilaya na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Barua hiyo ambayo ilisainiwa na mtu anayeitwa Kabungo ilihusu utaratibu wa kupata mikopo kwenye taasisi za fedha.

“Mnaombwwa kuwataarifu watumishi walioko chini yenu, kuwa kuanzia sasa mtumishi atakayehitaji mkopo kwenye taasisi za fedha pamoja na mahitaji mengine ya taasisi hizo, ili kupata mkopo, atatakiwa pia kuwasilisha uthibitisho wa kama hana mkopo wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, maombi ambayo hayataambatana na uthibitisho, hayatashughulikiwa,” iliosema barua hiyo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo