Majaliwa amsaka faru John kwa DNA


Mwandishi Wetu, Arusha

Kassim Majaliwa
SIKU 10 baada ya kupokea taarifa inayoeleza utaratibu uliotumika kumhamisha faru John kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko Hifadhi ya Grumeti, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imeunda timu kuchunguza utaratibu huo, ikiwa ni pamoja na kutafuta kaburi alikozikwa.

Majaliwa amesema timu hiyo ya wataalamu tayari imeshafika Sasakwa VIP Grumet kwa ajili ya kutafuta kaburi la faru huyo aliyeripotiwa kufa, kuchukua vinasaba vya masalia yake na kisha kwenda Hifadhi ya Ngorongoro kuchukua vinasaba vya watoto wake na kuvilinganisha na pembe ambazo alipelekewa kama ushahidi wa kifo cha faru huyo.

Kauli hiyo ya Waziri Mkuu imefufua upya sakata hilo baada ya Desemba 9 mwaka huu kupokea taarifa ya kuhamishwa kwa faru huyo ambaye Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema alihamishwa kwa sababu ya kupunguza tatizo la 'Inbreeding' ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Katika maelezo yake wakati akisoma taarifa hiyo iliyoandaliwa na Kamati ya Taifa ya kuwalinda tembo na faru, Waziri Maghembe alisema Julai 10, 2016 afya ya faru John ilianza kuzorota na alikufa Agosti 18 mwaka huu.

Sakata hilo liliibuka Desemba 6 mwaka huu, ambapo akiwa ziarani mkoani Arusha, Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), umletee nyaraka zote zilizotumika kumhamisha faru maarufu kwa jina la 'John' kutoka kwenye hifadhi hiyo, ndani ya siku mbili.

Alitoa agizo hilo alipotembelea ofisi za makao makuu ya NCAA zilizoko wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha na kuzungumza na watumishi wa mamlaka hiyo pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafugaji, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.

Kitendo cha jana Waziri Mkuu kuibua tena suala hilo ni wazi kuwa kutawapa wakati mgumu watendaji wa mamlaka zilizohusika kumhamisha, sambamba na kutoa taarifa za awali, ikiwemo pembe za faru huyo kuthibitisha kifo chake.

Akizungumza wakati wa majumuisho ya iliyolenga kukagua utekelezaji wa shughuli za maendeleo na kuona utoaji wa huduma kwa wananchi Majaliwa alisema, "Tume niliyounda kwa ajili ya uchunguzi wa faru John imetua VIP Grumet Serengeti kujiridhisha kama kuna kaburi la faru John na kama lipo wachukue vinasaba na baada ya hapo watakwenda Creter na kuchukua vinasaba vya watoto wa faru John na kuvipima kwa pamoja.

Lengo ni kutaka kubaini kama pembe iliyowasilishwa kwangu Disemba 9 mwaka huu ni ya faru John.”

"Wakati faru John akiwa V I P Grumet taarifa zilisema ni mgonjwa na daktari alipompima mara ya kwanza akabaini faru huyo hakuwa na ugonjwa wowote. Daktari alimpima tena kwa mara ya pili taarifa zikasema tena si mgonjwa ghafla wakasema amekufa. Hili haliwezekani."

Waziri Mkuu amesema ameiagiza timu hiyo kufanya kazi ya uchunguzi wa taarifa hizo kikamilifu kwa sababu Serikali imetumia fedha nyingi kuwaleta faru hao kutoka nchini Afrika Kusini. "Ni lazima nyara hizo za Serikali zilindwe kwa manufaa Taifa."

Awali, wakati akipotea taarifa ya faru huo Waziri Majaliwa alisema itafanyiwa kazi jambo ambalo linaashiria kuwa kazi hiyo imeshaanza kufanyika kutokana na agizo alilolitoa jana.

Alichokisema Maghembe

Wakati akiwasilisha taarifa hiyo Waziri Maghembe alisema, hadi kufikia Desemba 2015 wakati faru John anahamishwa alikuwa na watoto 26 (sawa na asilimia 70.2) ya faru wote waliokuwepo ndani ya kreta.

“Kati ya faru 37 waliokuwepo ndani ya kreta, watoto wake walikuwa 26 sawa na asilimia 70.2. Uamuzi wa kumuondoa John ulikuwa ni muhimu ili kuwezesha kuongezeka kwa faru weusi na kupunguza tatizo la ‘inbreeding’ ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro,” alisema Waziri Maghembe.

Baada ya kuhamishiwa Sasakwa, Waziri Maghembe alisema Julai 10, 2016 afya ya faru John ilianza kudorora na alikufa tarehe 18 Agosti, mwaka huu. Taarifa hiyo iliandaliwa na Kamati ya Taifa ya Kuwalinda Tembo na Faru.

Kamati hiyo inaundwa na Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI, Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Mkurugenzi Mkuu wa NCAA na Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro.

Akikabidhi pembe za faru huyo mbele ya Waziri Mkuu, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori, Robert Mande alimweleza kwamba pembe kubwa ya faru John ilikuwa na uzito wa kilo 3.6 na pembe ndogo ilikuwa na uzito wa kilo 2.3.


Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo