Lema sasa kula Krismasi gerezani


Seif Mangwangi, Arusha

Godbless Lema na mkewewakiwa mahakamani
RUFAA ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), kupinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha uliomnyima Mbunge huyo dhamana, imepangwa kusikilizwa Desemba 28.

Wakili wa Lema, Sheck Mfinanga alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa rufaa hiyo imepangwa kusikilizwa mbele ya Jaji Salma Maghimbi.

Kutokana na hali hiyo ni dhahiri kwamba Lema atakula Krismasi akiwa mahabusu ya Gereza Kuu la Kisongo ambapo Wakili Mfinanga alisema katika rufaa hiyo, watakuwa na hoja sita za kupinga uamuzi huo wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Rufaa hiyo itasikilizwa baada ya Mahakama hiyo Desemba 20 chini ya Jaji Modesta Opiyo, kukubali maombi ya Lema ya kutaka kuongezewa muda kwa ajili ya kuwasilisha notisi ya nia ya kukata rufaa ili isikilizwe.

Dk Opiyo alitoa siku 10 kwa mawakili wa mbunge huyo kuwasilisha notisi hiyo ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Arusha Novemba 11.

“Baada ya kupitia kwa kina uamuzi wa Jaji Mfawidhi Fatuma Masengi wa kukataa maombi yenu ya rufaa kwa kuwa yalikuwa nje ya muda, nimebaini kwamba kulikuwa na siku mbili za mapumziko, ambazo zilisababisha rufaa yenu kuonekana nje ya muda, kwa kuwa Mahakama haifanyi kazi siku za mapumziko.

“Kutokana na Mahakama kuridhishwa na sababu hizo, inawapa mawakili wa Lema siku 10 muwe mmeshawasilisha notisi ya kukata rufaa," alisema Dk Opiyo, Desemba 20.

Baada ya kauli hiyo, upande wa Serikali ukiongozwa na Mwanasheria Mwandamizi Elizabeth Swai, akisaidiwa na Adelaide Kassela; ulikubaliana na uamuzi huo pamoja na mawakili wa Lema; Mfinanga akisaidiwa na James Milya.

Awali maombi hayo namba 69 yaliwasilishwa mahakamani hapo chini ya hati ya dharura na Wakili Mfinanga chini ya kifungu 361(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Upande wa utetezi uliamua kuwasilisha maombi ya kukata rufaa kutokana na kutoridhishwa na uamuzi unaotarajiwa kukatiwa rufaa wa Novemba 11  kwenye  Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa  Arusha, chini ya Hakimu Desderi Kamugisha, ambako Lema anakabiliwa na kesi za uchochezi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo