Waziri aagiza daraja la Mbutu likamike haraka


Mwandishi Wetu, Mara

Profesa Makame Mbarawa
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amewapa miezi minne wakandarasi wazawa wa Kampuni ya Ujenzi ya Daraja la Mbutu JV inayojenga barabara ya Makutano hadi Nata wilayani Serengeti mkoani Mara kukamilisha kilomita 18 kati ya 50 za barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

Mbarawa alitoa agizo hilo, alipokuwa akikagua mradi huo wa barabara inayoanzia makutano kupitia Butiama, Nyamuswa hadi Sanzate ambao upo katika mkoa wa Mara na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wake ambayo imesuasua kwa takriban miaka mitatu sasa.

"Nataka mwezi Aprili mwakani sehemu ya barabara hii iwe imeshakamilika kwa kiwango cha lami na wananchi waanze kufurahia matunda yake. Hatuwezi kusubiri kwa muda wote huo kuwavumilia kukamilisha mradi huu”, alisema.

Alisisitiza kuwa nia ya Serikali ya kuboresha barabara hiyo ni kupunguza gharama za usafirishaji, kuboresha makazi, kukuza uchumi kwa maeneo yaliyo kando ya barabara hiyo na kuhamasisha utalii kwenye mbuga za wanyama za Serengeti na Ngorongoro.

Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads), mkoa wa Mara, mhandisi Japherson Nnko alisema kuwa barabara hiyo itakapomalizika itakuwa na njia ya magari yenye upana wa mita 6.5, mabega ya barabara ya mita 1.5 kila upande na Daraja kubwa la Kyarano lenye urefu wa mita 37.5.

Katika hatua nyingine, Serikali imesema itawapa kipaumbele makandarasi wazawa kuweza kushiriki katika mradi wa ujenzi wa reli mpya ya kisasa (Standard Gauge), inayotarajiwa kuanza hivi karibuni katika maeneo mbalimbali nchini.

Aidha, Serikali imewataka makandarasi hao kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa kwa kuomba zabuni za ujenzi huo na kuziimarisha kampuni zao, ikiwemo kuwa na vifaa vilivyo bora ili kupambana na soko la kibiashara na makandarasi wa nje.

Sambamba na hayo, waziri amekagua Uwanja wa Ndege wa Musoma na kusema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha inapanua na kujenga kwa kiwango cha lami uwanja huo, hususani njia ya kuruka na kutua ndege kutoka kilomita 1.6 ya sasa hadi kilomita 1.8 ili kuruhusu ndege kubwa zenye uwezo wa kubeba abiria 70 kutua.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo