Wananchi waua ‘panya road’ Dar


Dotto Mwaibale

WANANCHI wa Mbagala Sabasaba wamemuua kwa mawe na kumchoma moto kijana aliyetuhumiwa kujihusisha na uhalifu wa kundi maarufu jijini Dar es Salaam la ‘panya road’. Mbali na kijana huyo ambaye hakupatikana jina, wenzake wawili kati ya zaidi ya 15 waliokuwa pamoja walijeruhiwa mpaka kupoteza fahamu.

Mauaji hayo yalifanyika jana saa 11 jioni katika eneo hilo baada ya vijana hao kukurupushwa kutokana na madai ya kufanya uhalifu maeneo ya sabasaba Magengeni na Mbagala Zakhem.

Polisi walifika eneo la tukio na kulazimika kutumia risasi za moto kutawanya wananchi, kabla ya kuchukua mwili wa kijana huyo.

Akizungumza na mwandishi wa Jambo Leo, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye alijitambulisha kwa jina moja la Khalfan, alidai kuwa usalama wa wananchi upo mashakani kutokana na vitendo vya kundi hilo la ‘panya road’.

“Hawa ‘panya road’ walikuwa zaidi ya 15 wakitokea Mbagala Zakhem ambako walikuwa wakikimbizwa na wananchi baada ya kufanya uhalifu na walipofika hapa Sabasaba, walizingirwa na wananchi ambapo watatu kati yao walishambuliwa na mmoja kapoteza maisha baada ya kuchomwa moto,” alidai.

Alidai vijana wawili kati yao walijeruhiwa vibaya na kupoteza fahamu lakini wenzao wengine walifanikiwa kukimbia kwenda maeneo ya Yombo Dovya, huku wakiahidi kurudi kulipiza kisasi cha kuuawa kwa mwenzao.

Mkazi mwingine wa Mbagala kwa Mangaya, Seif Mwarami alidai vijana hao wataendelea kuuawa na wananchi kwa kuwa kila wanapokwenda kutoa taarifa Polisi, hawachukuliwi hatua yoyote badala yake wanaachiwa na kurudi mitaani kuendeleza uhalifu.

Alidai kuwa vijana hao wana umri mdogo ndio maana hawapelekwi mahakamani kutokana na kulindwa na sheria za watoto, jambo linalowatia hasira wananchi na kuamua kujichukulia hatua mkononi.

Kwa mujibu wa madai ya Mwarami, vijana hao wamekuwa wakitokea maeneo ya Kitunda, Moshi Baa na Yombo kwenda kufanya uhalifu Mbagala.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, Kamishna Msaidizi (ACP), Gilles Muroto alipopigiwa simu jana jioni alisemaalikuwa kwenye mkutano hivyo apigiwe baadae.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo