Mfuko wa wakfu kuendeleza korosho wafungwa


Jacquiline Mrisho – Maelezo

Dk Charles Tizeba
SERIKALI imesimamisha shughuli za Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza Zao la Korosho ili kupisha uchunguzi wa matumizi ya fedha za mfuko huo.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya mfuko huo kushindwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu pamoja na kuwepo kwa malalamiko ya muda mrefu kuhusu utendaji wake.

Uamuzi huo umetangazwa jana Dar es Salaam na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na changamoto ya zao hilo.

Dk. Tizeba alisema kuwa lengo la uanzishwaji wa mfuko huo lililoafikiwa na Serikali na wadau wa korosho limekuwa halifanani na utekelezaji wake, kwani maendeleo yote yanayoonekana kwenye zao hilo hayatokani na uwepo wa mfuko bali yanatokana na nguvu ya Serikali.

“Baada ya kutafakari utendaji wa mfuko huo tumegundua kuwa mfuko umeshindwa kutimiza malengo yaliyodhamiriwa, umeshindwa kusimamia na kutekeleza maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Bodi ya Korosho hivyo tumeamua kusitisha shughuli za mfuko huo na kuanzia leo shughuli hizo zitatekelezwa na Bodi ya Korosho mpaka hapo tutakapotoa maelekezo mengine.”alisema Waziri huyo.

Waziri aliongeza sababu nyingine za kusitishwa kwa Mfuko huo ni kujihusisha na vitendo vinavyohujumu wakulima wa zao hilo hasa wakati wa ununuzi wa pembejeo pamoja na kununua viuatilifu vilivyo chini ya kiwango kwa bei kubwa, matumizi mabaya ya fedha kinyume cha Sheria na Kanuni za mfuko pamoja na kushindwa kutekeleza agizo la Serikali kwa kuweka fedha kwenye amana za muda maalumu katika Benki mbalimbali badala ya kupeleka Benki Kuu.

Aidha, Dk. Tizeba alimtaka Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania anapowasilisha fedha zilizokusanywa na watu wanaosafirisha korosho nje ya nchi kuwasiliana kwanza na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho ili kufahamu usimamizi na utaratibu wa fedha hizo.


Kwa upande mwingine, Dk. Tizeba ameizuia Menejimenti ya mfuko huo kufanya muamala wowote wa fedha za mfuko mpaka hapo maelekezo ya hatima yao yatakapotolewa na badala yake miamala yote itafanyika kwa utaratibu utakaopangwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Aliiagiza Bodi ya Korosho kusimamia kwa haraka jukumu la upatikanaji wa pembejeo na viuatilifu kwa sababu msimu wa zao hilo umekaribia.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo