Mawakili wa Lema wapewa siku 10 za rufaa


Seif Mangwangi, Arusha

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Arusha chini ya Jaji wa Mahakama hiyo, Dk Modesta Opiyo, imetoa siku 10 kwa mawakili wa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kuwasilisha notisi ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Arusha, Novemba 11.

Uamuzi huo wa Jaji Opiyo ulitokana na maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na wakili wa Lema, Shack Mfinanga akiomba   kumwongeza mteja wake muda wa kuwasilisha notisi ya kukata rufaa hiyo.

“Baada ya kupitia kwa kina uamuzi wa Jaji Mfawidhi Fatuma Masengi ambako maombi yenu ya rufaa yalikataliwa kwa kuwa nje ya muda, nimebani kulikuwa na siku mbili za mapumziko ambazo zilisababisha rufaa yenu kuonekana kuwa nje ya muda, kwa kuwa Mahakama haifanyi kazi siku za mapunziko,” alisema na kuongeza:

“Kutokana na Mahakama kuridhishwa na sababu hizo, inawapa mawakili wa Lema siku 10 muwe mmeshawasilisha notisi ya kukata rufaa.”

Baada ya maagizo hayo, upande wa Serikali chini ya Mwanasheria Mwandamizi, Elizabeth Swai akisaidiwa na Adelaide Kassela walikubalina na uamuzi huo pamoja na Mfinanga akisaidiwa na James Milya.

Awali maombi hayo namba 69 yaliwasilishwa mahakamani hapo chini ya hati ya dharura na wakili Mfinanga chini ya kifungu 361(2) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.

Upande wa utetezi uliamua kuwasilisha maombi ya kukata rufaa kutokana na kutoridhishwa na uamuzi wanaotarajia kuukatia rufaa uliotolewa Novemba 11 na  Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa  Arusha iliyokuwa chini ya Hakimu Desderi Kamugisha.

Lema ambaye alikamatwa Novemba 2 mwaka huu Dodoma, hadi sasa anashikiliwa na Gereza Kuu la Kisongo, Arusha, kutokana na kusudio na Mkurugenzi wa Mashitaka ya Kupinga Uamuzi wa Hakimu Mkazi, Desdery Kamugisha aliyempa dhamana Lema katika kesi namba 440 na 441/2016 ya kutoa lugha za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo