Uvuvi wachangia asilimia 3 ya Pato la Taifa


Suleiman Msuya

SEKTA ya uvuvi nchini, imetajwa kuchangia asilimia 2.4 ya pato la Taifa wakati ukuaji wake ukiwa wa kasi ya asilimia 5.5.

Katibu Mkuu Wizara Mifugo, Kilimo na Uvuvi, Sekta ya Uvuvi, Dk Yohana Budeba alisema hayo jana kwenye mahojiano maalumu na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Alisema sekta ya uvuvi ni muhimu katika uchumi wa nchi, hivyo inapaswa kupewa msukumo mkubwa.

Dk Budeba alisema kwa sasa sekta hiyo inagusa kundi kubwa la jamii, hivyo mkakati ni kuona mchango wake kwa jamii na nchi unaongezeka kwa kasi kubwa.

Alisema mwaka jana, tani 42,000 za samaki ziliuzwa na kuiingizia Serikali Sh bilioni 7.5.

Dk Budeba alisema katika kuboresha sekta hiyo na wavuvi kuvua kwenye maji marefu, samaki watapatikana kwa wingi kama Serikali italipia asilimia 40 ya gharama za injini na vikundi vya wavuvi kulipia asilimia 60.

Alisema Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya chakula cha samaki kwa vikundi vya wavuvi, ili kuwaongeza nguvu na kuwapunguzia gharama.

"Mwaka jana, ilitoa Sh milioni 440 zilizonunua boti za kuvulia na kugawiwa kwa vikundi vya wavuvi," alisema.

Alisema pia ada ya leseni ya uvuvi imepunguzwa hadi Sh. 50,000 kwa mwaka na wavuvi wana uwezo wa kukata leseni ya miezi mitatu au sita.

Aliwataka wavuvi kujiunga na vikundi ili wapate elimu ya uvuvi wa kisasa, ruzuku na mikopo ya benki.

Katibu Mkuu huyo alisema Serikali imeanzisha kikosikazi kinachojumuisha wizara tano ili kukabiliana na uvuvi haramu, aliosema kuwa unatishia uwepo wa samaki na viwanda vidogo.

Dk Budeba alisema pamoja na changamoto zilizopo, sekta ya uvuvi imetoa ajira ya kudumu kwa wavuvi 185,000.

Hali kadhalika Serikali imejenga vitotoleshi vya samaki, ili kusaidia Watanzania kupata mbegu bora za samaki na mwitikio wa ufugaji samaki wa kisasa ni mkubwa.

Katibu Mkuu alisema Serikali inatarajia kujenga bandari ya uvuvi ili kuboresha sekta ya uvuvi nchini.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo