Mtoto Dar atoroka kwao akikimbia kukeketwa


*Ni mmoja kati ya 85 waliookeketwa, kufichwa majumbani

Dotto Mwaibale

MTOTO mwenye umri wa miaka 12 ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kivule katika Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam (jina linahifadhiwa) ameelezea jinsi alivyofanikiwa kuwatoroka wazazi wake ili asikeketwe.

Mtoto huyo hivi sasa analelewa na msamaria mwema baada kufungua kesi katika Kituo cha Polisi cha Stakishari Ukonga kufuatia kufikishwa kituoni hapo kwa ajili ya kujisalimisha na kuelezea madhila aliyotaka kufanyiwa.

Wakati mtoto huyo akijisalimisha katika kituo hicho, kuna taarifa za ndani kuwa kuna mpango wa kuwakeketa watoto 85 wenye umri kuanzia miaka 12 hadi 15 katika manispaa hiyo ambapo watoto zaidi ya 30 wanaeleezwa kuwa tayari wamekeketwa.

Akizungumza na JAMBOLEO, mtoto huyo alisema hawezi kurudi nyumbani kwao akihofia kupigwa na kukeketwa, badala yake anaomba msaada wa hifadhi kutoka kwa Watanzania.

"Baada ya baba yangu kufariki nyumbani kwetu Tarime tulikuja na mama hapa Dar esSalaam kwa kaka yake Chacha Nyanchiri anayeishi Kitunda Kivule karibu na Shule ya Msingi Misitu" alisema mtoto huyo.

Alisema katikati ya wiki iliyopita alifika bibi yake mzaa baba aliyemtaja kwa jina moja la Boke na kuwaambia yeye na wenzake wajiandaa kwenda kukeketwa.

Mtoto huyo alisema kwamba Alhamisi majira ya saa mbili usiku wakiwa nyumbani kwa mjomba wao anakoishi na mama yake, alifika bibi mzaa mama yake aliyemtaja kwa jina moja la Debora, huku akiwa ameongozana na mama yake na kuwaambia yeye na watoto wengine wawili wa mama yake mkubwa wakaoge ili waende kukeketwa.

Alisema ili kukwepa kukeketwa alipokwenda bafuni alifanikiwa kutoka na kupita njia nyingine na kufanikiwa kuwatoroka wazazi wake na kwenda kujificha kwenye pagala na ilipofika saa tatu usiku, alifika eneo la kwa Mpemba akielekea darajani ambako alikutana na dada mmoja aliyemsimulia mkasa huo.

Alisema dada huyo alimchukua hadi nyumbani kwake ambako alilala na siku iliyofuata alimpeleka kituo cha Polisi cha Stakishari kwa ajili ya usalama wake.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo ambaye alikataa kutaja jina lake alisema kuna mpango wa kuwakeketa watoto 85 kabla ya kuisha kwa mwaka huu wa 2016 na kuwa karibu watoto 30 wamekwishakeketwa.

Alisema shughuli hiyo inasimamiwa na wazee wa kimila wa kabila la Kikurya na kuwa ngariba mkuu wa kazi hiyo ya kukeketa watoto hao yupo eneo la Nyamuhanga na kuwa baada ya kukeketwa hufanyiwa sherehe kwa siri katika baadhi ya nyumba zilizopo jirani na ngariba huyo.

Mwenyekiti wa Serikali wa mtaa anaoishi mtoto huyo, Dominick Mlimi alisema hana taarifa ya mtoto huyo kutoweka nyumbani kwao.

"Jana niliwaona baadhi ya watoto wa kike wa familia ya Nyanchiri wakiwa hapo barabarani, lakini kuhusu kutoweka kwa mtoto huyo kwa kuhofia kukeketwa sijazipata" alisema Mlimi.

Mke wa Chacha Nyanchiri ambaye anaishi na mtoto huyo Regina Wilson alikiri mtoto huyo kuondoka usiku baada ya kufika nyumbani hapo bibi yake na mama yake ingawa alisema hawakutoa taarifa kwa mtu yeyote ya kutoweka kwake.

"Mwenye mamlaka ya mtoto huyo ni mama yake ambaye ametoka asubuhi kwenda kumtafuta mtaani, mimi sihusiki naye na wala sijui walichomwambia, ingawa siku zote tulipokuwa tukizungumzia kuhusu kukeketwa mtoto huyo alikuwa akionesha hofu," alisema Wilson.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Salum Hamdun alisema hakuwa na taarifa kuhusu tukio hilo ingawa aliahidi kuwasiliana na wasaidizi wake ili kulifuatilia na baadaye kutoa taarifa kamili.

Mtoto huyo alisema watoto wenzake waliofanyiwa vitendo hivyo bado wapo majumbani mwao wakijiuguza majeraha na kama vyombo vya usalama vitahitaji kwenda kuwaonyesha walipo yupo tayari.

Taarifa ambazo tumezipata jana kutoka kwa baadhi ya wananchi wanaoishi jirani na nyumba aliyokuwa akiishi mtoto huyo na mama yake, zimeeleza kuwa polisi walifika katika nyumba hiyo na kumkamata Regina Wilson, mama wa mtoto huyo Happyness na watu wengine wawili na kupelekwa kituo cha polisi Stakishari kwa mahojiano.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo