NIT yatakiwa kuchangamkia fursa sekta ya anga


Mary Mtuka

CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), kimetakiwa kuchangamkia fursa za kuandaa wataalamu wa kada mbalimbali za usafirishaji wa anga, ili kuinua sekta hiyo na kuiwezesha nchi kujulikana kimataifa.

Akizungumza Dar es Salaam juzi katika uzinduzi wa Baraza la Chuo hicho, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema kuzalisha wataalamu pekee haitoshi.

Alifafanua kuwa ni jukumu la uongozi wa Baraza hilo, kusaidia wataalamu hao kwa kuwaunganisha na mashirika makubwa ya usafirishaji.

Profesa Mbarawa aliutaka uongozi wa Chuo hicho kuweka mifumo imara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), ili kuwajengea mazingira mazuri walimu na wanafunzi.

Alisema lengo ni kuwajengea uwezo wasafirishaji hao katika kuhakikisha wanatambulika kimataifa na kujitangaza zaidi.

“Tayarisheni wataalamu na muwakutanishe na wakurugenzi wakuu wa kampuni kama Emirates, Qatar na Etihad, ili muwawezeshe kupata fursa kirahisi kwa kuonekana kimataifa,” alisema Profesa Mbarawa.

Alikitaka chuo hicho kuchukua wafanyakazi kutoka Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na kuwapa mafunzo ili kuzalisha wataalamu wenye ujuzi na uwezo wa kujenga miradi, ikiwamo ya ujenzi wa reli ya kisasa.

“Msipotumia fursa kama hizi kuandaa wataalamu, tutakosa watalaamu wazawa wa miradi mikubwa na kuanza kulalamika kuwa chuo kipo lakini hakithaminiki, kumbe mwanzoni tulishindwa kujipanga,” alisema.

Profesa Mbarawa alisema Baraza lililopita lilikuwa na uwezo wa kukusanya mapato ya ndani yatokanayo na ada za wanafunzi kutoka Sh bilioni 2.1 mwaka wa fedha 2011/12 hadi Sh bilioni 5.1 mwaka 2015/16.

Pamoja na mafanikio hayo, aliutaka uongozi kupunguza idadi ya kozi na kuwa na chache zenye tija na soko kimataifa, ili kufanya chuo hicho kuwa cha kipekee Afrika.

Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Zakaria Mganilwa alisema chuo kitaendelea kuandaa wataalamu mahiri na waliobobea katika sekta ya uchukuzi na usafirishaji na kuomba Serikali kuendelea kusaidia kuboresha miundombinu yake.

Mwenyekiti wa Baraza hilo, Profesa Bavon Nchomba alimhakikishia Waziri kuwa changamoto zote zinazokabili chuo, zitashughulikiwa kwa kuanzia na upunguzaji kozi zisizo na tija.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo