Aliyetelekeza mchumba kanisani ajirudi, amwoa


Moses Ng’wat, Mbeya

BWANA harusi Samwel Mwakalobo, aliyetelekeza Bibi harusi, Given Mgaya kanisani Ijumaa iliyopita, Desemba 16, amerejea kanisani na mwenzake huyo na kufunga ndoa, huku akisema alipoteza ufahamu wake aliposusa kwenda kanisani siku hiyo.

Mwakalobo na Given walikula kiapo cha uaminifu katika ndoa yao jana saa 9.38 alasiri kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Isanga jijini hapa, mbele ya Mchungaji Andangile Mwakijungu na baadaye kukabidhiwa vyeti vyao, baada ya Mwakalobo kwenda kumwomba ndoa yao iendelee.

Mapema asubuhi mwandishi wa JAMBO LEO alipigiwa simu na Mwakalobo akimwomba afike nyumbani kwake kwa mazungumzo, baada ya Bwana harusi huyo kushindwa kuzungumzia suala hilo tangu siku ya tukio, wiki iliyopita.

Alipofika, Mwakalobo alimkaribisha katika ibada ya ndoa hiyo, ambapo alikwenda kwenye Kanisa hilo, ambapo alishuhudia Mwakalobo na Given wakitangazwa kuwa wanandoa halali, kwa mujibu wa taratibu za KKKT na sheria za Tanzania.

Akielezea ilivyokuwa baada ya kufunga ndoa hiyo, Mchungaji Mwakijungu alisema alifuatwa na Mwakalobo kumwomba ampe nafasi ya pili ya kutimiza ahadi yake ya ndoa kwa mchumba wake Given.

Akisimulia tukio hilo baada ya kuruhusiwa na Mchungaji mbele ya mashuhuda, Mwakalobo alisema hakuwa akijitambua tangu Ijumaa ya wiki iliyopita hadi Jumatatu wiki hii.

Alisema baada ya kujitambua, alikimbilia kwa Mchungaji Mwakijungu kumwomba msamaha kwa yaliyotokea na kusema yalikuwa mapito na anajuta kukosa madhabahu ya Mungu.

Akizungumza ibadani hapo, Mchungaji Mwakijungu aliyetumia zaidi ya saa moja na nusu, alitoa wosia kwa maharusi hao na kuonya waumini waliokuwa wakizungumza mambo yasiyo ya ukweli, kuhusu tukio hilo.

Wazazi wa pande mbili walipopewa nafasi ya kuzungumza, walielezea namna tukio hilo lilivyowaimarisha, huku waumini wakisema: “Huyu ndiye Mungu anayeishi.”

Given aliyekuwa na wakati mgumu wiki iliyopita, aliwaomba msamaha waumini wote kwa niaba ya familia yake mpya na mumewe, na kuongeza kuwa wataendelea na maisha yao.

Desemba 16, Given ambaye ni mkazi wa Chimala, Mbarali, alikutwa na mkasa huo unaoelezwa kuwa mgumu zaidi katika maisha ya binadamu; wa kuachwa na mumewe mtarajiwa, siku ya harusi.

Given alipata taarifa mbili muda mfupi baada ya kutoka saluni, ambako alikuwa akipambwa tayari kwa ajili ya kwenda kanisani, lakini haikuwa rahisi kuziamini mpaka alipokwenda kuhakikisha kanisani.

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili kwa masharti la jina lake kuhifadhiwa, mmoja wa wapambe wa Bibi harusi alidai kuwa walipata taarifa ya kwanza muda mfupi baada ya kutoka saluni.

Kwa mujibu wa madai ya mpambe huyo, walimpigia simu Mwakalobo kumpa taarifa kuwa wako tayari; kwamba Bibi harusi na wapambe wake wameshapambwa tayari kwenda kanisani.

“Tulishangazwa na Bwana harusi, kwani alitujibu kwa mkato kuwa hawezi kuendelea na tumpeleke Bibi harusi kwa wazazi wake, akakata simu,” alisimulia mpambe huyo.

Mshangao huo ulisababisha wampigie simu Mwakalobo kwa mara ya pili ili kupata uhakika, ambapo mpambe huyo alidai simu ya Bwana harusi haikupatikana.

Wakati wakiwa kwenye taharuki, mpambe huyo alidai kuwa walipata taarifa ya pili, baada ya Mwakalobo kutuma ujumbe mfupi wa maandishi, akithibitisha kauli yake kuwa ameahirisha ndoa na ameshaondoka Mbeya kwenda Tunduma.

Kwa mujibu wa mpambe huyo, walikwenda kanisani na kutokana na hali hiyo, Mchungaji Mwakijungu alilazimika kutangazia waumini hao waliokuwa wakisubiri kushuhudia kiapo cha ndoa kwa vijana wao, kuwa ibada hiyo imeahirishwa bila kutamka siku itakayofungwa.


Sherehe

Licha ya mkasa huo ambao ni nadra kutokea duniani kuibua maswali mengi, ndugu wa upande wa mwanamume na wageni waalikwa ambao katika harusi za siku hizi mialiko hutolewa kwa waliochanga, waliendelea na sherehe iliyokuwa imeandaliwa.

Sherehe ya harusi ilipangwa kufanyika kwenye ukumbi mmoja jijini Mbeya, ambapo ilipotimu saa mbili usiku, wageni waalikwa na ndugu wa upande wa mwanamume waliwasili tayari kwa sherehe.

Mwandishi wa gazeti hili alifika ukumbini hapo, na kabla ya kuanza kwa sherehe hizo, mshereheshaji alialika mwakilishi wa familia ya upande wa Bwana harusi kueleza kilichojiri.

Akizungumza kwa niaba ya familia ya ndugu wa Bwana harusi, msemaji wa familia hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Joseph, aliwaomba radhi waalikwa na kuwataka wachukulie tukio hilo kuwa ni mapito tu.

“Mkiwa wazazi hakuna jambo jema kama kumpa zawadi mtoto wenu halafu akawashukuru,” alisema mwakilishi huyo bila kutoa ufafanuzi wa zawadi na shukrani na akaendelea:

“Naomba radhi sana kwa yaliyotokea, naomba tuzidi kuwaombea vijana wetu kuhusu shetani aliyeamua kujinyanyua juu yao,” alisema Joseph kwa niaba ya familia ya Mwakalobo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo