Wanasiasa watilia shaka uteuzi wa JPM


Waandishi Wetu

Dk John Magufuli
WAKATI Rais John Magufuli akiendelea kuteua makada na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa watendaji katika Serikali yake, vyama vya upinzani nchini vimeonya kuwa utaratibu huo unaweza kuzaa viongozi wanaotoa  matamko na uamuzi wa kukilinda chama hicho tawala badala ya taifa.

Aidha, vyama hivyo vimeeleza kwamba jambo hilo ni matokeo ya kuwa na Katiba inayompa Rais madaraka makubwa, vikitolea mfano baadhi ya wateule hao wanavyorumbana  na wapinzani kila kukicha ambapo wamemshauri Rais huyo kuteua zaidi wataalam wasiojipambanua kama wafuasi wa chama chochote cha siasa.

Hata hivyo, akizungumza wakati wa mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM hivi karibuni, Rais Magufuli alitetea uamuzi wa kuteua wanaCCM kwenye nafasi mbalimbali akisema ndio watu anaowafahamu na kwamba CCM ndiyo imepewa ridhaa ya kuongoza nchi.

Katika mahojiano na JAMBO LEO kwa nyakati tofauti, juzi viongozi wa vyama hivyo vya upinzani walisema kwamba licha ya watumishi wa Serikali kuwa na itikadi tofauti za siasa, hawawezi kulinganishwa na watendaji wengine wanaoingia Serikalini wakijulikana ni wanachama wa CCM na wengine wanaotokea kwenye uongozi ndani ya chama hicho.

Juzi Rais Magufuli aliteua wakuu wa wilaya wawili, wakurugenzi watatu wa Mamlaka za Serikali za mitaa na wenyeviti saba wa Bodi za taasisi huku Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma  na Utawala Bora, Angela Kairuki akiteua makatibu tawala wa wilaya 27 kujaza nafasi zilizokuwa wazi.

Lakini wanasiasa hao walidai kuwa uteuzi huo ni mwendelezo ule ule wa siasa za CCM ambapo walimtaja Diwani wa Kata ya Kiloka (CCM) Robert Selasela ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Kilombero kuwa ni mfano wa watendaji hao.

Hata hivyo, akizungumzia suala hilo Kairuki alisema: “Kwani sheria za madiwani zikoje? Mstahiki Meya Kinondoni alipokuwa katika nafasi hiyo hujui kuwa alikuwa anafanya kazi TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania).”

Katika maelezo yake Selasela alisema: “Udiwani sio kazi ya kudumu, lakini pia nitaona wakubwa watakavyoshauri. Mambo haya yana kanuni za utumishi na za viongozi. Nitaangalia miongozo yote na mwisho wa siku nitafanya uamuzi sahihi ambao hautaathiri upande wowote. Ila kwa sasa mawazo yangu yote yapo Kilombero.”

Wanasiasa
Katibu Mkuu wa Chama cha Wakulima (AFP), Rashid Rai alisema: “Anachokifanya Rais ni kuteua watu watakaolinda maslahi fulani na kupambana na wapinzani katika maeneo wanayoyaongoza.”

“Mfano ni Jimbo la Arusha, kuna mvutano mkali kati ya Lema (Godbless-Mbunge wa Arusha Mjini-Chadema) na Gambo (Mrisho-Mkuu wa mkoa Arusha). Rais anasema yeye ni wa watu wote ila mbona anateua wa chama chake tu?”

Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi alisema: “Wanapelekwa zaidi katika maeneo ambayo wapinzani wana nguvu ili wakapambane nao na kumaliza nguvu zao za kisiasa.”

Huku akitolea mfano wa Jimbo la Arusha, Muabhi alisema kada wa CCM akiwa Katibu Tawala hawezi kukubali kupitisha jambo linaloonekana wazi kukiminya CCM, hata kama lina maslahi katika sehemu husika.

Alifafanua: “Yamekuwa mazoea kwa awamu zote kuwa na watu wa aina hii ili kuvunja upinzani. Lazima aweke watu wa chama chake, tena baadhi ndio wanaokuja kuwa wasimamizi wa changuzi mbalimbali.”

Alisema ni vigumu kuwa na uhusiano mzuri kati ya wateule hao wa Rais na wabunge wa upinzani katika maeneo mbalimbali nchini.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro alisema: “Tumefikia hapa kutokana na kuwa na Katiba mbovu ambayo inampa Rais mamlaka makubwa bila mtu mwingine kuhoji, kwa mfano uteuzi wa makatibu hawa haujabainishwa wazi wanapaswa kuwa na sifa zipi bali kama mteuzi anaridhika nao anaweza kuwachagua.”

Alidai kwamba baadhi ya wateule hao huwa vinara wa kuharibu chaguzi mbalimbali huku akitolea jinsi wakurugenzi wa halmashauri walivyovuruga chaguzi za mameya, ukiwemo wa Meya wa Kinondoni.

Naye Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Danda Juju aliungana na Mtatiro huku akitaja maeneo ambayo wateule hao wa Rais wanalumbana na wabunge na madiwani wa upinzani.

Ends
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo