Wanawake waongoza kwa Ukimwi


Dotto Mwaibale

UTAFITI umeonesha kuwa wanawake ndio waathirika wakubwa wa maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwa Tanzania Bara wakilinganishwa na wanaume.

Hayo yalielezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Dk Leonard Maboko wakati akitoa taarifa jana kwa waandishi wa habari kwenye mkutano wa kujitambulisha kwao tangu ateuliwe na Rais John Magufuli kushika nafasi hiyo Julai 7.

Alisema maambukizi ya VVU kwa Tanzania Bara ni asilimia 5.3 wanawake wakionesha kuathirika zaidi kwa asilimia 6.2 dhidi ya wanaume ambao ni asilimia 3.8.

"Utafiti huo wa mwaka 2011 na 2012 ulionesha kuwa mkoa wa Njombe ulikuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ukiwa na asilimia 14.8 ukifuatiwa na Iringa asilimia 9.1 na Mbeya asilimia 9," alisema Dk Maboko.

Dk Maboko alisema Manyara ulikuwa na kiwango kidogo cha maambukizi ya asilimia 1.5 lakini takwimu za ndani ya mkoa huo eneo la Mirerani kwenye mgodi wa TanzaniteOne, maambukizi ya VVU yalikuwa ni asilimia 16 kiwango ambacho ni cha juu ya mkoa wa Njombe.

Dk Maboko aliomba wananchi kokote waliko kutobweteka kwa mafanikio ya mapambano dhidhi ya VVU na Ukimwi yawe endelevu hata katika maeneo au mikoa ambako kuna maambukizi madogo ya VVU.

Alisema nchi inatakiwa kuweka nguvu nyingi kifedha na kimkakati kwenye maeneo na makundi yenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU ikiwa ni pamoja na kuimarisha utafiti na ukusanyaji takwimu za VVU na Ukimwi ili kuendelea kubaini na kupanga mipango dhidi ya ugonjwa huo inayoongozwa na takwimu.

Aliongeza kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloratibu mapambano dhidi ya Ukimwi (UNAIDS) limeweka malengo ya muda wa kati ya tisini tatu (90-90-90).

90 ya kwanza inamaanisha asilimia tisini ya watu wote wanaokisiwa kuwa na VVU kujua hali zao na 90 ya pili ikimaanisha kuwa asilimia tisini ya waliobainika kuwa na VVU kuanza kutumia dawa za kupunguza makali ya VVU (ARVs) mara moja na 90 ya tatu ya walioanza dawa waweze kuwa na ufubazo endelevu wa virusi vya Ukimwi mwilini.

Dk Maboko alitoa mwito kwa wananchi, taasisi za kijamii, Serikali, watu binafsi na kampuni za kibiashara kuchangia mfuko wa udhamini wa masuala ya ukimwi (ATF) ulioanzishwa na Serikali ili kuondokana na utegemezi kwa wafadhili.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo