Tume ya Uchaguzi yapata Mwenyekiti mpya


Mwandishi Wetu

Balozi John Kijazi
RAIS John Magufuli amemteua Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Semistocles Kaijage, kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na wengine sita katika nyadhifa tofauti na wanatarajiwa kuapishwa leo.

Jaji Kaijage anachukua nafasi ya Jaji mstaafu Damian Lubuva ambaye muda wake wa kuwa Mwenyekiti ulimalizika rasmi Desemba 19.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, kupitia Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Gerson Msigwa ilieleza kuwa Jaji Kaijage aliteuliwa kuongoza Tume hiyo kwa miaka mitano kuanzia Desemba 20.

Aidha, Rais Magufuli alimteua Jaji mstaafu Hamid Hamid kuwa Makamu Mwenyekiti wa NEC kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Jaji mstaafu Hamid alikuwa Makamu Mwenyekiti wa NEC na kumaliza kipindi chake cha kwanza cha miaka mitano Desemba 19.

Hali kadhalika, alimteua Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Harold Nsekela kuwa Kamishna wa Maadili katika Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa miaka mitano kuanzia Desemba 20.

Jaji mstaafu Nsekela anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji mstaafu Salome Kaganda aliyestaafu  Desemba 10.

Katika hatua nyingine, Rais aliteua majaji wanne wa Mahakama Kuu kuwa majaji wa Mahakama ya Rufaa ambao uteuzi wao ulianza jana na ni majaji Dk Gerald Ndika, Jackobs Mwambegele, Rehema Mkuye na Sivangilwa Mwangesi. Wateule hao wanatarajiwa kuapishwa leo Ikulu, Dar es Salaam.



Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo