Moto wazuka ofisi ya DC Same


Joyce Anael, Same

MOTO mkubwa umezuka katika maeneo ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro na kusababisha hasara kubwa.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na baadhi ya mashuhuda, moto huo ulianza majira ya saa moja na nusu usiku Jumamosi iliyopita ukianzia katika ofisi za usajili wa vyeti vya vizazi na vifo Rita.

Walisema moto huo uliziteketeza kabisa ofisi za Uhamiaji, Rita, ofisi ya mshauri wa mgambo, stoo na masjala.

“Umeme ulikuwa umekatika na uliporudi, ghafla niliona moto mkubwa ukitokea kwenye ofisi za Rita na kuenea kwenye ofisi zingine na ndipo nikaanza kufanya mawasiliano ambayo yalipelekea wananchi kujitokeza kwa wingi kutoa msaada”, alisema mlinzi aliyekuwa zamu siku ya tukio, Kighono Saidi.

Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Sitaki Senyamule amesema athari kubwa iliyotokea ni kutokana na ukosefu wa huduma ya zimamoto wilayani humo.

“Tulitoa taarifa ya moto huu mapema, lakini hakuna huduma ya zimamoto katika wilaya yetu wala wilaya jirani ya Mwanga na hili limechangia athari kubwa,” alisema.

Alisema ili kupata ufumbuzi wa haraka ilibidi gari la zimamoto litokee mjini Moshi ambako ni umbali wa zaidi ya kilomita 100 kutoka wilayani Same na kwamba lilichukua takribani saa mbili kufika mjini humo na kukuta athari kubwa ishatokea.

Rosemary aliendelea kusema kuwa kuna haja ya kuwepo kwa huduma hizo kila wilaya ili kuepuka athari za namna hiyo zisitokee tena wakati mwingine.

Aliwapongeza wananchi waliojitokeza kuuzima moto huo ambao hata, hivyo alisema ulikuwa ukikua kwa kasi kutokana na mazingira ya upepo mkali yaliyoko katika wilaya hiyo.

Katibu tawala wa mkoa wa Kilimanjaro, Aisha Amour aliyefika eneo la tukio na kujionea hali ilivyo, alisema kuna haja ya miundombinu ya umeme kuangaliwa upya katika majengo yote ya serikali mkoani humo.

Aidha alitoa muda wa siku mbili kwa TEMESA, kwa ushirikiano na TBA na idara ya zimamoto kumpa taarifa ya madhara yaliyotokana na moto huo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo