Mtu azikwa na kuku, kondoo

Francis Godwin, Iringa 

MAMIA  ya  wakazi  wa Kijiji  cha  Mbigili na  mji  wa Ilula  katika  Wilaya ya  Kilolo mkoani Iringa, wamefurika katika mazishi  ya aina  yake  yaliyofanyika katika kitongoji  cha Mkawaganga  Kijiji  cha Mbigili  Wilaya ya  Kilolo mkoani Iringa  kushuhudia mazishi ya  kihistoria ya mzee mmoja aliyefariki  dunia ghafla na  kuzikwa kaburi  moja na kondoo na  kuku mweusi.

Tukio   hilo  limetokea  jana wakati  wa mazishi ya mzee huyo, Andrea Ngaga (90) mkazi wa kitongoji  cha Mkawaganga  aliyekuwa  akijishughulisha na kazi  za uganga  wa kienyeji kijijini  hapo enzi  za  uhai  wake .

Baadhi ya  wananchi  waliofika katika mazishi  hayo  walisema  kuwa  walilazimika  kusitisha   shughuli  zao za  shamba na biashara na  kufika  kushuhudia  mazishi hayo ambayo ni mara ya kwanza  kufanyika katika  kijiji  hicho.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, John  Mfaligoha  alisema kuwa  kabla ya  kifo chake marehemu  aliwaeleza  namna mazishi yake alivyotaka yawe.

Kwa sababu kulikuwa na taarifa hizo, wananchi wakatamani kufika ili waone aina hiyo ya mazishi, alisema.

Mwenyekiti  wa  Serikali ya  Kijiji  cha Mbigili,  Ibrahim  Rashid (46)  alisema  amezaliwa katika  kijiji  hicho miaka mingi, lakini tukio hilo ni la kwanza  kuliona na kusikia.

Hata hivyo alieleza kuwa mazishi hayo  yamefanyika kimila  zaidi na mara nyingi mahala pengine marehemu anachagua mtu  wa  kuzikwa naye  kabla ya  kifo .

“Huyu (marehemu) hakuweka maagizo, alisema tua angetamani kuzikwa kimila na hizo ndizo mila za eneo hili,” alisema mwenyekiti huyo wa kijiji na kubainsha kuwa aliyeongoza  mazishi hayo ni mganga  wa kienyeji  kutoka Ifunda  wilaya ya  Iringa aliyemtaja kwa jina la  Galasiano Mfaume Nyeza  ambaye  ni baba mdogo  na marehemu  huyo.

Mtendaji  wa Serikali ya  kijiji hicho, Thabith  Kalolo  alisema  kimsingi  hakuna kosa  lolote, kwani serikali haiingilii uhuru wa  wananchi  wake kuamini masuala ya  mila na kuwa   iwapo mazishi hayo yangekiuka haki  za  binadamu mwingine; mfano  kama wangemzika  na  binadamu mwingine aliyehai, hapa isingewezekana  ila  kwa kumzika na kondoo na kuku  mweusi hakuna  shida .

Hata   hivyo,  alisema tofauti  ya  rekodi ya misiba iliyopata  kutokea  katika  kijiji  hicho, msiba huo umevunja rekodi kwa  kuhudhuriwa na idadi kubwa ya  watu.

“Tumezoea rambirambi za misiba kuwa ni kati ya Sh300,000 na Sh500,000, lakini msiba huo rambirambi zimefika Sh1.3 milioni. Hii ni dalili kwamba msiba huu umekusanya watu wengi sana,” alisema.

Mtoto  wa marehemu, Kurugenzi Ngaga  alisema  kuwa baba yake  alifariki  dunia juzi  saa 6 usiku baada ya kusumbuliwa na  chembe  ya moyo. Alisema marehemu ameacha  wajane   wawili na watoto 19.

Kurugenzi alisema  kimila kama  ingekuwa  zamani,  marehemu  angezikwa na mjukuu wake  aliyemteua kushika mikoba yake,  ila  kutokana na mambo  ya mila kwa  sasa kupewa kisogo, waliona ni  vema wakamzika na kondoo na kuku  huyu  mweusi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo