Acheni kujisaidia porini—DC

John Banda, Bahi

MKUU wa Wilaya ya Bahi, Elizabeth Kitundu amewataka wakazi wa wilaya hiyo kuacha kujisaidia porini, badala yake wajenge vyoo vya kisasa kwa ajili ya kujilinda na magonjwa ya milipuko.

Kitundu aliitoa kauli hiyo jana kwenye maadhimisho ya Siku ya Unawaji Mikono Duniani iliyoambatana na kufikia ubora wa usafi wa mazingira katika Vijiji vya Zanka na Mayamaya wilayani Bahi.

Miradi hiyo ya usafi wa mazingira wilayani humo inatekelezwa na Shirika la Plan International chini ya Mradi wa Usafi wa Mazingira Tanzania (Umata).

Kitundu alisema katika Wilaya ya Bahi kuna  Kata 22 na vijiji 59 na kwamba ni wajibu wa wenyeviti na watendaji kuhakikisha kaya zilizopo eneo hilo zinaacha kujisaidia porini na zijenge vyoo vya kisasa.

Alisema kujenga vyoo vya kisasa pamoja na kunawa mikono anapotoka chooni ni jambo la lazima kwa wakazi wa wilaya hiyo.

“Tatizo kubwa lipo katika Kijiji cha Mayamaya, kaya 758 hazina vyoo na 348 zilikuwa na vyoo. Natoa agizo tujenge vyoo vya kisasa pamoja na kunawa mikono tunapotoka chooni,” alisema

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Programu ya Umata kutoka Shirika la Plan Internation, Judith Maire alisema lengo ni kuwa na jamii safi hasa Dodoma iwe katika mazingira safi na salama.

Judith alisema programu ya Umata inatekelezwa katika Wilaya za Mkoa wa Dodoma ambazo ni Bahi, Chamwino na Kongwa, huku uchaguzi wa Wilaya hizo ukizingatia hali hafifu ya usafi wa mazingira na magonjwa ya milipuko kulinganisha na wilaya zingine.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo