Mpoki Bukuku kuzikwa leo Dodoma


Sharifa Marira na Peter Akaro

Marehemu Mpoki Bukuku
ALIKUWA mwandishi wa habari wa aina yake. Ndivyo unavyoweza kueleza kutokana na jinsi watu wa kada mbalimbali, wakiwemo viongozi walivyomzungumzia Mpigapicha wa magazeti ya The Guardian Ltd, Mpoki Bukuku aliyefariki dunia Ijumaa.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe waliongoza mamia ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam wakiwemo waandishi wa habari kuaga mwili wa marehemu huyo katika viwanja vya shule ya sekondari Tabata Wazazi, huku wakisema tasnia ya habari imepata pigo kwa kumpoteza mwanahabari aliyemudu kufanya kazi bila uoga, licha ya kukumbana na vikwazo mbalimbali.

Bukuku alifariki saa chache baada ya kugongwa na gari jirani na kituo cha mabasi cha ITV Mwenge, wilayani Kinondoni, wakati akitoka kazini kuelekea nyumbani kwake Tabata Kimanga.

Mwili wa Bukuku ulisafirishwa jana kuelekea Dodoma ambako utazikwa leo.

“Tasnia ya habari imepoteza mtu muhimu aliyetoa mchango mkubwa kwa taifa kupitia taaluma ya habari. Waandishi wa habari tumepoteza mtu muhimu kilichobaki sasa ni kupitia kazi zake na kujifunza mazuri yote aliyoyafanya wakati wa uhai wake,” alisema Nape.

Alibainisha kuwa umati wa wanahabari uliohudhuria kumuaga Bukuku ni ishara kwamba wakati wa uhai wake alifanya kazi zake kwa weledi mkubwa.

Kwa upande wake Mbowe alisema Taifa limempoteza mtu ambaye alikuwa mstari wa mbele kuandika habari zenye kujenga nchi.
“Katika kumuenzi marehemu, waandishi wa habari wanatakiwa kufanya kazi bila ya woga kwa kukosoa kwa lengo la kujenga taifa,” alisema Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni.

“Simamieni ukweli katika kuandika habari na msiogope wala kutishwa kwa sababu wananchi wanawategemea nyinyi kupaza sauti zao.”

Mkurugenzi Mtendaji wa The Guardian Ltd, Richard Mgamba alisema kampuni imepata pigo kutokana uchapakazi na ucheshi na akaiomba familia kuvumilia katika kipindi hiki kigumu

“Mpoki alipoacha kazi Mwananchi (gazeti linalochapishwa na Kampuni na Mwananchi Communication Ltd) baada kama ya miezi miwili alinipigia simu na kuniambia kuwa hana kazi. Kutokana na kutambua uwezo wake nilimwambia aje na kumweleza kuwa hastahili hata kufanyiwa usaili,” alisema Mgamba.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari (Moat), Said Kubenea alieleza jinsi anavyomkumbuka marehemu, huku akikumbushia tukio la Bukuku kupigwa na askari magereza eneo la Ukonga wakati wakifuatilia baadhi ya askari hao waliovamia nyumba za wafanyakazi wa lililokuwa Shirika la Ndege Tanzania (ATC).

“Kwa namna alivyochaniwa nguo na kulowa damu siku ile inaonyesha alikuwa anafanya kazi kwa maslahi ya umma bila ya woga,” alisema.

“Kifo cha Bukuku ni pigo kwa tasnia ya habari. Wakati wanahabari wakiomboleza kifo wakuu wa wilaya wamekuwa wakiwanyanyasa waandishi wa habari,” alisema Deodatus Balile, Mwakilishi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

“Tunawaonya wakuu wa wilaya wanaowaweka mababusu na kuwapigisha magoti wanahabari waache kwa kuwa lengo la wanahabari ni kusema ukweli daima bila kupendelea,” alisema.

Naye, Msemaji wa familia,Alfred Mwakapesya alisema Bukuku aliyezaliwa Machi 15, 1972 ameacha mke na watoto watatu.

Alishukuru jamii ya wanahabari, madaktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa msaada wao katika kipindi hicho kigumu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo