Kesi ya ‘Scorpion’ yanguruma


Jemah Makamba

KESI dhidi ya Salum Njwete ‘Scorpion’ anayedaiwa kumjeruhi kwa kumtoboa macho Saidi Mrisho, imeendelea kusikilizwa kwenye Mahakama ya Wilaya ya Ilala kwa mashahidi wawili wa upande wa Jamhuri kutoa ushahidi.

Shahidi namba mbili, Stara Sudi ambaye ni mke wa mlalamikaji na shahidi namba tatu, Yahya Kisukari anayetajwa kuwa mdogo wa Mrisho, walitoa ushaidi wao mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Flora Haule wakiongozwa na Wakili wa Serikali, Nasoro Katuga.

Wakili Katuga alianza na maswali kwa shahidi namba mbili kabla ya kuhitimisha kwa shahidi namba tatu, huku Mahakama hiyo ikishuhudia Wakili wa mshitakiwa akishindwa kumuuliza Stara maswali.

Wakili: Shahidi unaishi wapi na unafanya kazi gani?

Shahidi 2: Naishi Mabibo Makuburi na ni mama wa nyumbani.

Wakili: Ulifunga lini ndoa na mume wako ambaye ni mlalamikaji?

Shahidi: Nilifunga ndoa na mlalamikaji mwaka jana mwezi wa 10.

Wakili: Unakumbuka tarehe sita mwezi wa sita mwaka huu nini kilitokea?

Shahidi: Nilikuwa nimelala usiku, nikapigiwa simu na kusikia sauti ya mume wangu akiniambia yuko Buguruni na amechomwa visu na ametobolewa macho, haoni.

Wakili: Uliwezaje kujua kuwa hiyo ni sauti ya mumeo?

Shahidi: Niliweza kujua kutokana na kuniita jina la Mama Hance na nikaitambua sauti yake, ambapo simu iliita tena nikasikika mtu mwingine akisema twende Amana haraka.

Wakili: Baada ya hapo, ulichukua hatua gani wewe kama mke?

Shahidi: Nilitoka mimi, mama yangu na dada yangu tukaelekea Amana Hospitali.

Wakili: Ieleze Mahakama mlimkuta mgonjwa katika hali gani?

Shahidi: Tulimkuta akiwa amewekwa bandeji kwenye macho na pamba kwenye majereha ya mgongoni na tumboni.

Wakili: Je, uliweza kumhoji amefanya nini majeraha hayo?

Shahidi: Niliweza kumuuliza, alinijibu amechomwa visu na mtu ambaye hamjui, lakini aliweza kusikia watu wakimtaja kwa jina la Salum na Scorpion.

Wakili: Baada ya hapo nini kiliendelea hospitali ya Amana?

Shahidi: Mgonjwa alihamishwa kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kwa matibabu zaidi.

Wakili: Wewe kama mke, baada ya hapo na kutajiwa jina la aliyemfanyia tukio, yeye alichukua hatua gani?

Shahidi: Nilikwenda Buguruni Kituo cha Polisi na kutoa taarifa nikapewa askari wa kike, nikaenda naye Muhimbili ambako alimhoji mgonjwa na baada ya kutajiwa jina la mtuhumiwa, akasema tuondoke wakamkamate.

Wakili: Baada ya hapo nini kiliendelea?

Shahidi: Nilifika hospitali siku ya tatu na kukuta madaktari ambao walisema mgonjwa wetu hawezi kuona.

Wakili: Uliishi na mume wako tangu mwaka jana, uliwahi kusikia ana tuhuma zozote za wizi au kukamatwa na Polisi?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Je, hakuwa na kazi nyingine zaidi ya kinyozi?

Shahidi: Hapana, hakuwa na kazi nyingine.

Wakili wa Serikali alimaliza maswali na kuiachia Mahakama kama ina lolote ambapo wakili wa utetezi, Juma Nassoro alisema hana swali kwa shahidi huyo ambapo shahidi wa tatu alianza kutoa ushahidi wake.

Wakili: Shahidi unafanya kazi gani?

Shahidi 3: Kinyozi saluni ya Rogerz, Tabata Sanene.

Wakili: Hujawahi kusikia tuhuma zozote za wizi kwa mlalamikaji?

Shahidi: Hapana sijawahi.

Wakili: Una muda gani hapa mjini?

Shahidi: Miaka minne.

Wakili: Mlalamikaji ni kaka yako kivipi?

Shahidi: Tumezaliwa na mama mmoja, baba tofauti.

Katika kesi hiyo, wakili wa Scorpion alimhoji maswali shahidi huyo namba mbili na sehemu ya mahojiano hayo ni kama ifuatavyo:

Wakili: Unapafahamu Buguruni?

Shahidi: Sipafahamu.

Wakili: Kwa nini wewe na ndugu yako mnakana kupafahamu Buguruni, mnaogopa nini?

Shahidi: Sipafahamu ila huwa napita tu.

Wakili: Wewe unajua Kiswahili vizuri? Kwa nini unasema hupafahamu halafu unasema huwa unapita tu?

Shahidi: Sijawahi kushuka Buguruni.

Wakili: Hujawahi kwenda na kaka yako Buguruni kununua simu?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Mara ya mwisho kuuza simu saluni kwenu ilikuwa lini?

Shahidi: Hatujawahi kuuza.

Baada ya maswali hayo, wakili wa utetezi alisema amemaliza maswali huku upande wa Wakili wa Serikali akiiomba Mahakama iwapangie siku nyingine ya kuendelea na ushahidi.

Hakimu Flora aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 11 kuendelea na ushahidi huku mshitakiwa akirudishwa rumande.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo