Watuhumiwa wa ujambazi watatu wauawa na wananchi


Joyce Kasiki, Dodoma

WATU watatu wanaosadikiwa kuwa majambazi, wameuawa na wananchi waliovunja sheria kwa madai ya hasira, baada ya wahusika kutuhumiwa kuteka na kupora fedha kwenye kituo cha mafuta cha Dabalo, Chamwino mkoani hapa.

Akizungumza na waandisi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Lazaro Mambosasa alisema mauaji hayo yalifanyika Jumatano saa tatu usiku kijijini Dabalo.

Alidai kuwa watuhumiwa hao wa ujambazi, waliokuwa na pikipiki mbili moja namba T 194 CQF na nyingine aina ya SunLG isiyo na namba, walipora Sh milioni 2.09.

Alisema baada ya kufanya unyang’anyi huo, taarifa zilifika kwa wananchi wa kijiji hicho na vijiji jirani ambao walianza msako porini na kufunga barabara kijijini Segala.

“Majambazi walipofika kwenye kizuizi hicho, waligeuza na kuelekea kijiji cha Manyemba ambako pia walikutana na kundi la watu, wakafyatua risasi na kuwajeruhi Nyembela Mganga mguuni na mkewe Ndalandala Nyembela, ambaye pia alijeruhiwa mguu; wote ni wakazi wa Manyemba,“ alisema Kamanda Mambosasa.

Alifafanua kuwa wananchi hao wakishirikiana na askari wawili wa kituo cha Polisi cha Dabalo, waliendelea na msako na kuwakuta watuhumiwa hao porini, ambapo waliwashitukia wananchi na kukimbilia Mlima Kinyami kijijini Hombolo, huku wakifyatua risasi angani kutishia wananchi.

Mambosasa alisema licha ya majambazi hao kufyatua risasi, wananchi hawakurudi nyuma ndipo nao wakakimbia pande tofauti baada ya kuishiwa risasi.

Alisema wananchi waliendelea na hatimaye kukamata watano na kati yao, watatu walishambuliwa na wananchi na kuwaua papo hapo.

Aliwataja waliouawa kuwa ni Johnas Mahanze ‘Chinaa’ mkazi wa Dakawa, Morogoro, Elias Kazembe wa Ifakara, Morogoro na mmoja aliyetambuliwa kwa jina moja la utani la Mzungu mkazi wa Kiteto, Manyara.

Alisema watuhumiwa waliokamatwa wakiwa hai ni Shaban Sefu wa Dumila na Mashaka John wa kijiji cha Kikombo-Dabalo, Chamwino na ndiye alikuwa mwenyeji wao.

Kamanda alisema watuhumiwa hao walikamatwa na bunduki tatu aina ya shotgun; moja iliyofutwa namba, magobori mawili na Sh 220,000 zilizokuwa sehemu ya mgao wa fedha walizopora.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo