Ujue ugonjwa wa tezidume


Dk. Stephen Kisaka

TEZI dume kitaalamu hujulikana kama Prostate Gland. Hii ni tezi ambayo ni kiungo kimojawapo katika mfumo wa uzazi wa mwanaume. Tezi dume ni sehemu mojawapo ya mfumo wa uzazi wa kiume. Tezi hii ndogo hupatikana ndani ya nyonga kwa maana ya kwamba ipo mbele ya puru na chini kidogo ya kibofu cha mkojo.

Tezi hii imeuzunguka mrija unaotoa mkojo katika kibofu ujulikanao kama urethra. Huhusika katika kutengeneza majimaji yajulikanayo kama semen.

Kuvimba kwa tezi dume au kama ijulikavyo kitaalamu Benign Prostate Hyperplasia au Hypertrophy au kwa kifupi chake BPH ni hali ambayo huwapata wanaume wenye umri mkubwa.

Kwa wengi huanza wakiwa na umri wa miaka ya kuanzia 50 na kuendelea kwa mujibu wa mtandao wa (www.nks.uk/conditions/prostate-enlargement/pages).

Chanzo hasa cha uvimbe huu hakijulikani vizuri ni nini ila inadhaniwa kuwa ni kutokana na mabadiliko ya homoni kadri umri unavyoongezeka Tezi dume ikiwa kawaida picha ya kwanza na picha ya pili ikiwa imevimba Tezi dume ikiwa kawaida Endapo sasa tezi hii itakuwa imevimba husababisha msukumo au pressure kuongezeka katika kibofu cha mkojo na njia ambayo mkojo hupita na hapo huweza kuleta madhara kama vile shida katika kuanza kujisaidia haja ndogo, kushindwa kukojoa kabisa, kutaka kujisaidia haja ndogo mara kwa mara na kushindwa kumaliza haja ndogo ndani ya kibofu wakati wa kujisaidia.

Mengine ni kuamka usiku mara kwa mara na kuwa katika hali ya kutaka kujisaidia, wakati mwingine huweza kukufanya kuona damu inatoka kwenye mkojo.

Baada ya muda tatizo hili pia huweza kukusababishia tatizo lingine la kuziba mkojo kabisa na hata mawe madogomadogo katika kibofu cha mkojo. Pia husababisha uambukizo wa mara kwa mara katika kibofu cha mkojo.

Madhara mengine ambayo pia yanaweza kuambatana na tatizo hili ni pamoja na tatizo la figo au kibofu cha mkojo, shinikizo la damu, kushindwa kutoa shahawa kwenye uume, damu kuganda na uambukizo ndani ya njia ya mkojo na kupata nimoni au homa ya mapafu.

Kwa baadhi ya wanaume dalili hizi zaweza kuwa ndogo na zisihitaji matibabu lakini kwa baadhi ya watu wengine dalili hizi huweza kuendelea na kufikia kuwa tatizo kubwa na kukupa usumbufu katika mfumo wa maisha yako.

Lakini kwa mujibu wa mtandao wa www.nhs.uk/condition/cancer-of-the-prostate/pages umeelezea kuwa tatizo la watu wenye uvimbe wa tezi dume haiwapi hatari kubwa ya kupatwa na saratani zaidi ya wale wasiougua tezi dume kupata saratani.

Uchunguzi
Ili uweze kugundulika kuwa una tatizo la tezi dume kulingana na sehemu au eneo ulipo hatua kadhaa za uchunguzi zinaweza kufanyika. Baadhi ya vipimo vinaweza kufanywa na daktari wako na vingine kufanywa na wataalamu wa idara maalumu kama vile ya mkojo.

Hatua za kufuata kulingana na aina ya hospitali au uwezo wa hospitali uliyopo. Daktari atakuuliza maswali na endapo utakuwa na dalili za ugonjwa huu wa tezi dume basi kitakachofuata ni kupangilia dalili hizo katika madaraja kama yalivyo katika mtiririko wa mpangilio wa dalili hizo kimataifa.

Unaweza kupewa karatasi ya kujaza baadhi ya maswali. Kila swali lina majibu na uzito wa jawabu hutumika kupima uzito wa ugonjwa wenyewe.

Mfano wa maswali, ambayo yanaegemea kipindi cha mwezi mmoja uliopita ni mara ngapi umejisikia kubakia na haja ndogo katika kibofu baada ya kumaliza kujisaidia?

Je ni mara ngapi umejisikia kwenda kujisaidia haja ndogo chini ya saa mbili tangu ulipomaliza mara ya kwanza? Je imekutokea au ni mara ngapi haja ndogo imeacha kutoka ghafla wakati unajisaidia na baadaye kuendelea kutoka tena?

Je ni mara ngapi imetokea shida kuahirisha kujisaidia haja ndogo? Je ni mara ngapi imekutokea kupata mkojo kidogo au usio na kasi ya kawaida katika kutoka? Je ni mara ngapi imekutokea kuamka usiku na kwenda kujisaidia haja ndogo?

Umuhimu wa kuulizwa maswali haya utamsaidia daktari wako kujihakikishia anayatenga magonjwa mengine yoyote yanayoweza kuwa au kukaribiana na dalili za ugonjwa wako.

Pia tukumbuke dalili za ugonjwa wa tezi dume zinafanana sana na dalili za saratani ya tezi dume hivyo daktari atapenda kujihakikishia kuwa tatizo lako sio saratani au la.

Vipimo
Katika ugonjwa huu wa tezi dume daktari atafanya vipimo kulingana na kadri atakavyoona yeye na baadhi ya vipimo ni pamoja na haja ndogo, haja kubwa kupitia kidole, ultrasound scan, CT scan na rekodi ya takwimu za haja ndogo.

Takwimu za kitaalamu zinaonyesha kuwa wagonjwa wengi wenye matatizo ya tezi dume wapo zaidi kwa wenye matatizo ya shinikizo la damu na kisukari, ijapokuwa kisukari na shinikizo la damu pia huambatana na hali ya kiasili ya mwili kadri umri unavyoongezeka (aging process).

Matibabu ya ugonjwa huu wa tezi dume hutegemeana na hali ya ugonjwa ulivyo nayo yapo katika makundi matatu ambayo ni:-

Kubadili mfumo wa maisha. Mfano kuepuka vinywaji walao masaa mawili kabla ya kwenda kulala ili kuepuka usumbufu wa kuamka usiku.

Kuepuka unywaji wa pombe au kahawa au punguza vitu hivi kwani huwasha kibofu cha mkojo na kufanya dalili kuwa mbaya zaidi.

Kufanya mazoezi kiasi kwa muda wa nusu mpaka saa moja, ni mfumo ambao umeonekana kwa kiasi fulani kusaidia tatizo kuongezeka.         

Njia nyingine ni ya kutumia dawa. Hapa daktari anaweza kuchagua dawa kulingana na hali ya mgonjwa na ataendelea kukufuatilia. Upasuaji ni hatua nyingine ya matibabu kulingana na hali ya ugonjwa baada ya vipimo kufanyika. Upasuaji hufanyika ili kurekebisha uvimbe huu wa tezi dume.

Kinga
Zipo baadhi ya tafiti zinazoonyesha kuwa ulaji mzuri wa vyakula vya jamii ya protein pamoja na mboga za majani zimeonyesha kwa kiasi kikubwa kupunguza uwezo wa kupatwa na tatizo hili.  Tahadhari nyingine ni ya kula vyakula vyenye mafuta mengi au nyama nyekundu. Baadhi ya vyakula ambavyo ni chanzo kizuri cha protein ni pamoja na mayai, maziwa, soya, samaki, karanga, nazi, matunda kama parachichi na kuku

Ushauri
Tunapaswa kutambua kuwa tatizo la tezi dume lipo na kwa kadiri umri unavyoendelea ndivyo unavyokuwa katika hali ya kupatwa na shida hii inaweza kuwa kwako au kwangu au kwa mtu yoyote yule. Unachotakiwa chukua tahadhari mapema kwa kuangalia afya yako kwa kufika hospitali kwa wataalamu na kupimwa ili kujijua kuwa haupo katika hali hii.

Wakati unapochelewa kufika hospitali na kukuta dalili zimeshakuwa sugu au ugonjwa kuwa mkubwa pia matibabu huchukua muda mpaka mgonjwa kurudi katika hali yake ya kawaida. Maoni au maswali tuma kwa simu

0713247889 au kwa baruapepe: afya@jamboleo.net
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo