Ukubwa Baraza la Mawaziri uelezwe Kikatiba


Abraham Ntambara

WANASIASA na wasomi, wameunga mkono ushauri wa mfanyabiashara maarufu nchini, Jaffar Sabodo kumtaka Rais John Magufuli kupunguza Baraza la Mawaziri, lakini wamesema ni vizuri suala la idadi ya mawaziri likawekwa kwenye Katiba ili liwe mwongozo kwa kila kiongozi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na JAMBO LEO jana walisema ushauri huo ni mzuri, lakini inatakiwa kuwekwa kikatiba ili kumdhibiti Rais anayetaka kuunda baraza hilo kulingana na maono yake.

Profesa Mwesigwa Baregu alikiri kuwa ushauri huo ni mzuri na kubainisha kuwa mwisho wa siku, hilo linabaki kuwa suala la Kikatiba.

Alibainisha kuwa Katiba ina uwezo wa kusema kwamba baraza la mawaziri lisizidi  idadi fulani ya mawaziri kwa kila Rais atakayeingia madarakani.

Hilo linatakiwa kuwa sharti la Kikatiba kama Rasimu ya Katiba ya Warioba ilivyokuwa imependekeza  kwamba Baraza lisizidi kiasi Fulani, alisema.

“Nadhani hiyo ndiyo inaweza ikasaidia kwa maana kwamba akija Rais na akataka kulipanua Baraza, hawezi kufanya hivyo kwa sababu Katiba inamdhibiti,” alisema Baregu.

Alisisitiza kuwa ukubwa wa Baraza la Mawaziri unatakiwa kuwa katika Katiba. inatakiwa iwe imeainishwa kama ilivyofanya  Rasimu ya Katiba ya Warioba.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) Taifa wa NCCR- Mageuzi, Samwel Ruhuza alisema Marekani ina wananchi zaidi ya milioni 250 wakati Baraza lao la mawaziri linaundwa na mawaziri wasiozidi 15.

Aidha aliongeza kuwa Uingereza nayo ina idadi ya watu takribani 150, lakini baraza lao la Mawaziri linaundwa na mawaziri 20.

“Hii maana yake ni kwamba hayo yote yapo kwenye Katiba, sasa uwingi wa mawaziri haina maana kwamba ndiyo kuna kuwa na ufanisi wa kazi,” alisema Ruhuza.

Alibainisha kwamba baraza linapokuwa dogo inakuwa rahisi katika kulisimamia. Alisema  Katiba tuliyonayo haimdhibiti Rais, hivyo inampa uhuru wa kuamua ukubwa wa baraza kulingana na yeye anavyotaka.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda alisema falsafa ya kubana matumizi kwa kuwa na baraza dogo la mawaziri imekuwa ikitumika sana hasa kwenye nchi zinazoendelea ikiwamo Marekani.

“Sasa kule Marekani hizo wizara zipo kisheria kabisa, lakini ni chache tu wala siyo nyingi nafikiri falsafa hiyo tunaweza kuitumia,” alisema Mbunda.

Aidha alisema kuwa cha msingi zaidi ni kuangalia kiwango chetu ambapo tunahitaji watu wa kusukuma maendeleo katika sehemu mbalimbali na kuongeza kwamba wakati mwingine si vyema kuwa na waziri mmoja kwenye wizara ambayo ni kubwa kama ya Kilimo na mifugo  kwani anaweza kushindwa kuzisimamia kiukamilifu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo