Serikali yaitaka TTCL izinduke


Mary Mtuka

Profesa Makame Mbarawa
SERIKALI imeitaka Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kujipanga kwa mkakati wa kutangaza huduma za fedha ambazo zitatolewa na kampuni hiyo mwakani.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, wakati akikagua mitambo itayotumika kwa huduma hiyo ambayo itaongeza ushindani wa biashara kwenye huduma za simu nchini mkoani Dodoma.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Profesa Mbarawa alisema kuna umuhimu wa kampuni hiyo kujipanga katika idara ya masoko kwa kutangaza huduma hiyo kwa njia zote.

"Ni lazima mjipange kwenye idara ya masoko kwa kutangaza huduma yenu kwa kutumia njia zote za mitandao ya kijamii, ili wananchi warahisishiwe huduma za fedha kupitia TTCL," alisema Waziri.

Aidha, aliitaka kampuni hiyo kujipanga kuona fursa zilizopo kwa kutambua mahitaji ya wateja wao na kuhakikisha inaongeza wateja mkoani humo ili kuteka soko la ushindani ambapo Serikali inajipanga kuhamia huko.

Alisema baadhi ya maeneo ambayo TTCL inahitaji kuboresha zaidi ni upande wa simu (voice) na data (video) ili kurahisisha mawasiliano kwa mikutano ya njia ya video kwa kuwa baadhi ya watendaji wengine watabaki Dar es Salaam.

"Naamini mkiimarisha mawasiliano upande wa data mtarahisisha hata uamuzi na pia kazi zitakwenda vizuri serikalini, hasa ikizingatiwa baadhi ya watumishi watakuwa Dodoma na wengine Dar es Salaam," alisema.

Pia Waziri Mbarawa alisema shirika hilo linapaswa kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ili kufikia malengo liliyojiwekea na kuendana na kasi ya utendaji wa Serikali.

Alimhakikishia Mkuu wa Mkoa, Jordan Rugimbana, kuboresha miundombinu ikiwamo usafiri wa anga katika uwanja wa ndege wa Dodoma ili kuruhusu ndege kubwa kuruka na kutua.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo