Ridhiwani ataka Sera ya Elimu kuwakomboa wahitimu


Venance Nestory

Ridhiwani Kikwete
MBUNGE wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete amesema Sera ya Elimu nchini inapaswa kuwaandaa vijana kujiajiri badala ya kutegemea kuajiriwa.

Alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa Mahafali ya 15 ya Chuo Kikuu cha Mzumbe tawi la Dar es Salaam.

Alisema kuna ulazima wa kubadili mifumo ya elimu nchini ili iweze kumkomboa kijana wa Kitanzania anayehitimu Chuo Kikuu badala ya kumfanya mtumwa wa ajira.

“Mfano kwa siku ya leo pekee, vijana zaidi ya 550, wametunukiwa Shahada za Umahiri na wengi wao hawana ajira ya kudumu, sasa kama viongozi wa taifa hili tuna mikakati gani ya kuokoa vijana wanaohitimu kila mwaka katika vyuo vyetu,” alihoji Ridhiwani.

Ridhiwani aliendelea “Ukiachana na hilo tuna dhana potofu miongoni mwetu hasa kutowapa nafasi mbalimbali vijana waliohitimu vyuo mbalimbali kwa kigezo cha kukosa uzoefu. Nawaombeni waajiri tuwape nafasi hawa vijana wajifunze na kuonesha uwezo wao.”

Ridhiwani alisema ni vyema hatua za haraka zikachukuliwa dhidi ya wahitimu kwa kuwapa mitaji ili kutatua janga la vijana wasio na ajira katika jamii inayotuzunguka.

Alisema suala hilo linapaswa kuwa na jamii nzima, ikiwamo taasisi za kifedha ambazo nazo zinapaswa kuwaamini vijana hao na kuwapa mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kuanzisha biashara.

“Nimebaini kuna vijana wenye uwezo mkubwa wa kufanya tafiti na wanatambua umuhimu wa mafanikio katika elimu zao ila hawana mitaji na wanahitaji kusaidiwa kifedha na vitendea kazi,” alisema.

Iwapo mazingira bora ya kujiajili yataandaliwa kwa vijana tutapunguza wimbi la vijana wasio na ajira mitaani na kuendana na Sera ya Serikali iliyopo madarakani ya kukuza uchumi wa viwanda. 

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo