AWT kunufaisha waendesha bodaboda, bajaji


Mwandishi Wetu, Dodoma

MFUKO wa Kuendeleza Hifadhi za Wanyamapori Afrika (AWT) umeahidi kusaidia upatikanaji wa Sh bilioni moja ili kutekeleza awamu ya kwanza wa kuimarisha mtandao wa Taasisi ya Huduma za Usafirishaji wa Pikipiki na Bajaji (Tamosa).

Upanuzi wa mtandao huo unahusisha mikoa ya Dodoma, Mara, Morogoro, Singida na Arusha.

Ofisa Mkuu Mwandamizi wa AWT, Pratik Patel alisema hayo hivi karibuni mjini hapa, kwenye mkutano wa Bodi ya Wadhamini wa Tamosa ambapo pia mikoa hiyo ilitajwa.

Mbali na kuongoza AWT, Patel pia ni mwakilishi wa taasisi za kimataifa za hifadhi ya mazingira zikiwamo za World Conservation Fund na African Wildlife Trust, zinazoendesha kampeni za kitaifa na kimataifa kuendeleza utalii na kudhibiti ujangili dhidi ya tembo.

Alisema waendesha bodaboda hawapaswi kuachwa nje ya mikakati ya kukuza uchumi wa Taifa, badala yake unahitajika usimamizi thabiti, mafunzo ya sheria za usalama barabarani na kuboresha huduma za usafiri huo.

“Bodaboda wanagongwa, wanapoteza viungo, wanakufa...AWT tutakaa na mshirika wetu, Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) na Tamosa kuangalia vipaumbele ili kuibua miradi ya kibiashara, elimu na uendeshaji wa bodaboda kwa usalama na kukuza uchumi wa Taifa,” alisema.

Kwa mujibu wa Patel, mkakati huo utahusisha Serikali ili kuchagiza kasi ya uboreshaji huduma za usafiri kwa kuendeleza madereva ili pamoja na mambo mengine, waipende na kuiheshimu sekta hiyo.

Katibu Mkuu wa Tamosa, Kizito Msangya alisema kama ushirikiano uliopo kati yao na mamlaka kama halmashauri za wilaya, manispaa na majiji, Polisi, Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) utaboreshwa, kutakuwa na ufanisi wenye tija kwa pande zote.

Msangya alisema katika kujiimarisha na kuboresha huduma zao, Tamosa inakusudia kusajili vituo vya bodaboda, kuanzisha miradi na kutoa mikopo ikiwamo ya pikipiki, ujenzi wa vituo vya mafunzo ya udereva na sheria za usalama barabarani, ili kuwajengea uwezo madereva na kupunguza ajali barabarani.

Mlezi wa Tamosa, Balozi Job Lusinde alisema kuwapo kwa bodoboda ni matokeo ya uamuzi wa Serikali kufungua fursa pana za ajira hasa kwa vijana.

“Hatua hii ilifungua mianya ya kibiashara ikiwamo soko la watengenezaji na wauza pikipiki na kuimarisha huduma ya usafiri wa haraka kwa nauli nafuu," alisema.

Lusinde alisema baada ya vijana wa Tamosa kufanya utafiti wa kina, ilionekana umuhimu wa kuunda taasisi hiyo na kupitia malengo ya Katiba yao, aliamua kuwaunga mkono na kuwa mlezi wao.

Mjumbe wa Bodi ya Tamosa kwa mkoa wa Dar es Salaam, Gaudens Mushi alisema ushirikiano baina ya taasisi hiyo na kampuni za kibiashara zikiwamo za mawasiliano ya simu za mkononi, utasaidia kuanzisha na kuendeleza kampeni ya elimu ya usalama barabarani.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo