Nec yasitisha uchaguzi kata za Mkoma, Mwamtani


Emeresiana Athanas

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imesitisha mchakato wa uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi za udiwani katika Kata za Mkoma na Mwamtani unaotarajiwa kufanyika Januari 22 mwakani.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Uchaguzi (NEC), Ramadhan Kailima, alisema kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya tume hiyo kujiridhisha kuwa kata hizo haziko wazi kisheria.

"Tume imefuatilia na kujiridhisha kuwa kata hizo ni kweli haziko wazi kwa mujibu wa sheria na hivyo kutoa maamuzi ya kuziondoa katika orodha ya kata zilizotangazwa kufanya uteuzi wa wagombea na kufanya uchaguzi,"alisema.

Alifafanua kuwa katika kata ya Mkoma iliyopo Halmashauri ya Rorya mkoani Mara, diwani alishindwa kesi yake katika mahakama ya chini na kuamua kukata rufaa mahakama ya juu, hivyo kuifanya nafasi hiyo kutokuwa wazi kwa kuwa uamuzi unaweza kubadilika na kuendelea kuwa diwani wa kata hiyo.

Aidha katika kata ya Mwamtani iliyoko Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, alisema diwani wake ana sifa za kuendelea kushikilia nafasi hiyo kwa mujibu wa sheria kutokana na kumaliza kifungo chake cha miezi sita.

"Diwani wa kata hii alihukumiwa kifungo cha miezi sita na tayari ametumikia kifungo hicho hivyo kwa mujibu wa sheria bado anasifa ya kuendelea kuwa diwani wa kata hiyo," alisema.

Kata hizo ni miongoni mwa kata 22 zilizotangazwa na tume hiyo kuwa zitafanya uchaguzi mdogo kujaza nafasi wazi za madiwani kwenye halmashauri mbalimbali Tanzania Bara.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo