Takukuru yasaka mikataba ya kampuni


Salha Mohamed

SERIKALI kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeanza msako wa mikataba ya kampuni zinazotakiwa kulipa kodi katika manispaa zake, ili kubaini ufisadi Dar es Salaam.

Hatua hiyo ya Serikali imefikiwa baada ya kampuni ya simu za mkononi ya Zantel, kulipa Sh milioni 687.9 kwa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kutokana na kuwapo madai ya ufisadi katika ulipaji kodi.

Fedha hizo zililipwa Desemba 21 na ni za kipindi cha miaka saba ambapo zilielekezwa katika ujenzi wa madarasa 40 katika Manispaa hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Hapi alisema tayari Takukuru inafanya uchunguzi wa waliohusika kuficha mkataba wa kampuni hiyo na kuisababishia Halmashauri kukosa mapato.

“Tumeanza msako na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, hatujali wanamlipa nani, watatulipa fedha zote wanazodaiwa na Serikali haiwawekei kinga na mashitaka, vyombo vya ulinzi vinaendelea na kazi yao nasi tunaendelea na kazi zetu,” alisema.

“Mkataba huo ambao haukuonekana kwenye kumbukumbu za Manispaa kwa maana ya kuibiwa na kushindwa kutuwezesha Kinondoni kupata mapato tangu mwaka 2009,” alisema.

Alisema alipata mkataba kutoka vyanzo vyake na kuwataka kulipa kiasi hicho ndani ya siku saba, huku vyombo vya ulinzi na usalama vikichunguza na kubaini mhusika aliyekuwa akilipwa fedha hizo, aliyeiba mkataba na kuuficha.

Alitoa rai kwa kampuni zilizoingia mkataba na Serikali anayedhani ameuficha au kuunyofoa kwenye kumbukumbu za Manispaa walianza msako kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.

Hapi alisema: “Takwimu zinaonesha mwaka huu idadi ya wanafunzi 19,000 walifaulu Kinondoni, na kuchaguliwa awamu ya kwanza ni 12,889 huku wanafunzi 3,169 wakikosa nafasi.”

Alisema wilaya ina upungufu wa vyumba vya madarasa 79, ambapo vyumba 40 vitajengwa kwa fedha hizo na kubaki upungufu wa 39.

Aliongeza kuwa watafanya tathmini ya kuwa na sifa ya kujiunga na sekondari huku akibainisha kuwa hadi Januari wahakikishe kila aliyefaulu anakwenda sekondari.

Hapi alisema: ”Nawaagiza wakurugenzi wote mkoani humu wajipange ili kuhakikisha wanatimiza na kutekeleza maagizo ya serikali yaliyotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

“Kila mtoto aliyefaulu anapata nafasi ya kupata elimu ya sekondari, hili ni wajibu wetu, wakurugenzi na manispaa zote kuhakikisha maagizo halali ya Majaliwa ili kuendelea kutekeleza nia njema ya Rais John Magufuli,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo