Kingunge: Uchaguzi mwaka 2020 mgumu


*Awashauri wapinzani kuhakikisha Katiba mpya inaandikwa
*Lowassa akubali yaliyopita si ndwele sasa aganga yajayo

Celina Mathew

Kingunge Ngombale-Mwiru
MWANASIASA mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru, ameupa upinzani mbinu za kushinda uchaguzi mkuu mwaka 2020 na kwamba bila hivyo wasahau kushika Dola huku akieleza kuwa mapambano kwa sasa ni makubwa.

Kingunge amewataka wapinzani kuhakikisha wanazifanyia kazi changamoto hizo kabla ya uchaguzi ambazo ni kuwapo kwa tume huru ya mabadiliko ya Katiba na sheria inayoruhusu matokeo ya uchaguzi wa rais kuhojiwa mahakamani.

Alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana alipokutana na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuzungumza na vijana wanaojiita wapenda mabadiliko, waliokamatwa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana kutokana na makosa mbalimbali na kusikiliza changamoto walizokutana nazo.

"Tunapopambana tuweke suala hilo karibu, tufanye yote lakini tuhakikishe tunapata Katiba mpya au vipengee vilivyo kwenye Katiba inayopendekezwa virekebishwe. Pia bila shinikizo kutoka kwa wananchi, Serikali haitakubali kutuachia nchi, hivyo tambueni mapambano ni makubwa, lakini tunayaweza," alisema.

Mwanasiasa huyo aliongeza kuwa kama kuna mtu anadhani anaweza kupata wema kwa kupewa na Mungu, shetani au miujiza amepotea, kwa kuwa kila kitu ni matokeo ya mapambano.

Alisema yeye alianza kutafuta mabadiliko siku nyingi akiwa sekondari na haikuwa rahisi kwake, kutokana na kuwa wengi walikuwa wasaliti na hawakufanya kitu.

Alisema hatua ya yeye kuacha kazi na kwenda kuitumikia TANU aligombana na baba yake, kwa kuwa hakupenda kitendo hicho hata kusababisha baba yake amnunie kwa miezi sita.

"Napenda niwaambieni, mabadiliko yanataka watu wenye moyo wa ujasiri, kwa maana mapambano ya sasa ni magumu zaidi, kwa kuwa mazingira yamebadilika hivyo inahitajika nguvu kubwa ya vijana kukabiliana nayo," alisema Kingunge.

Alisema, awali kulikuwa na utawala wa Wakoloni na Waingereza licha ya kuwa wanyonyaji na wakandamizaji, walikuwa na umoja wao, hawakupenda watu wajiunge na chama, lakini walikuwa wastaarabu.

"Jambo linaloshangaza ni kuwa watawala wetu hawaheshimu sheria wala Katiba, mtatendewa mabaya sana, hivyo muwe tayari kukabiliana nayo…hali ya sasa inahitaji vijana wenye moyo wa mabadiliko," alisema na kuongeza:

"Chadema inakubalika na Lowassa anakubalika, lakini katika mazingira ambayo kuna uongozi wa Serikali usioheshimu Katiba, inabidi jitihada zifanyike na kubwa zaidi," alisema.

Lowassa

Lowassa alisema yaliyopita si ndwele na kuwataka wapenda mabadiliko kuganga yajayo, kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Lowassa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alitumia fursa hiyo kuwapongeza kwa ujasiri na kuwashukuru kwa kuchagua mabadiliko.

Alisema yaliyopita walikubaliana nayo na kilichobaki sasa ni huhakikisha wanaunda jeshi kubwa, ili kuendelea na mjadala wa kushinda ifikapo mwaka 2020.

Aliwataka vijana hao kuhakikisha kuwa hawakati tamaa na kutumia changamoto walizopata kama mwanzo wa mafanikio.

"Tumejifunza kuhifadhi mafanikio hayo, hivyo nawaomba msikate tamaa kwa maana naamini uchaguzi uliopita tulishinda na unaokuja mwaka 2020 tutashinda tena kwa kishindo," alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo