Krismasi yaja na kilio cha Amani


Waandishi Wetu

Rais Magufuli kanisani
KAULI za kutaka Serikali, vyama vya siasa na wananchi kuombea amani ya nchi ni mambo yaliyotawala katika mahubiri ya ibada za mkesha wa Krismasi juzi na Krismasi yenyewe jana katika maeneo mbalimbali nchini.

Mbali na viongozi hao wa dini, Rais Magufuli akiwa katika Kanisa Kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu Mjini Singida, alisisitiza suala la amani, akisema ni muhimu kwa jamii yoyote inayopenda kupiga hatua katika maendeleo yake.

Walichosema maaskofu Maaskofu, wachungaji na mapadri wa makanisa mbalimbali walioendesha Ibada ya Krismasi walitumia muda mwingi kuhimiza amani, huku baadhi yao wakisisitiza kuwa siku zote amani huletwa na maskini wasio na kitu na sio matajiri.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliwataka watu kutambua kuwa amani ya kweli hailetwi na matajiri au watu wenye utawala na mamlaka ya ulimwengu, bali huletwa na maskini wasio na kitu.

Akitoa mafundisho katika mkesha wa Krismasi katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph juzi usiku, Kadinali Pengo alisema masikini mwenye hamu ya kupata utajiri ni hatari kuliko aliyerithi, iwapo atausaka utajiri huo kwa njia zisizo halali.

“Amani hailetwi na matajiri wenye fedha, majumba mazuri…, kila anayetaka amani anapaswa kutekeleza wajibu wake. Tukiomba amani tuwe wa kwanza kutekeleza majukumu na wajibu wetu ili tuwe chimbuko kwa jirani na ndugu zetu. Tunaodai amani tuwe wa kwanza kuwa mfano,” alisema.

“Si ufukara tu unaoweza kukuwezesha kuwa na amani, wapo masikini wengi wanaotafuta mali kwa njia yoyote ile wakidhani watakuwa na amani kumbe si kweli.

Haijalishi ni fukara kiasi gani kila mtu ana uwezo wa kuwa chimbuko la amani miongoni mwa watu, unapotafuta usiseme mimi ni maskini, sina uwezo wa kiutawala na kwamba huwezi kuwa na amani.”

Huku akisisitiza kuwa inaposakwa amani isitarajiwe kuwa italetwa na wenye fedha, wanaostarehe, wanaokunywa kuzidi uwezo wao, alisema watu wa kundi hilo wasitarajiwe kuwa ndiyo wasaka amani.

“Katika maisha ya sasa masikini ndio wanaokesha kulinda usalama wa nchi zao na wao ndio watakaopewa kipaumbele katika habari ya ukombozi. Masikini ndio wanaofanya kazi za matajiri kwa sababu hawajihusishi na anasa, hivyo matajiri wanapokuwa wamelala kwa kushindwa kufanya kitu kutokana na kulewa wao (masikini) hukesha wakifanya kazi,” alisema.

Alisema watu wengi hawaelewi sababu za Yesu Kristo kuzaliwa katika hali ya umasikini na kusisitiza kuwa jambo hilo ni fumbo kubwa kwani licha ya kuzaliwa katika familia hiyo, Yesu alihubiri neno la Mungu kwa masikini.

“Mungu anajiainisha kwa hao masikini na anaiainisha shughuli nzima ya ukombozi kwa kuanza nao, dhiki ya ulimwengu siku ya leo ni kwa kila wenye mapenzi mema maana mara nyingi tunadhani matajiri ndio wanaweza kuleta mali,”alisema Kadinali Pengo.

Malasusa atema cheche

Akizungumza katika Kanisa la Azania Front, Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa aliitaka Serikali na vyama vya siasa kudumisha amani iliyodumu kwa muda mrefu, kusisitiza “kamwe wasijaribu kuivunja.”

“Tunapaswa kuitunza bila kujali itikadi za kisiasa kwani ni zawadi ya kipekee ambayo Mungu ametupatia. Yapo mataifa ambayo hadi leo yanahangaika kuitafuta Amani ambayo sisi tunajivunia nayo, hii ni zawadi ambayo Mungu aliamua kuipatia Tanzania hivyo tuitunze,” alisema.

“Niwaombe viongozi wetu na wanasiasa kuendeleza mshikamano kwani ndio silaha kubwa ya ushindi.”

Katika ibada hiyo ambayo iliendeshwa na msaidizi wa Askofu huyo, Chidieli Luiza ilienda sambamba na utoaji wa zawadi baina ya waumini kwa waumini, pia Askofu Malasusa alitumia nafasi hiyo kutoa zawadi za kanisa kwa waumini.

Padri wa Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Alban, jijini Dar es Salaam, Johnson Lameck alisema, “Tunapaswa kudumisha amani na upendo katika mwaka ujao na tuhakikishe hatufanyi mambo yasiyofaa. Ujumbe wetu kama kanisa ni ‘amani’. Nchi yetu ni ya Amani tusiivuruge.”

Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony Lusekelo alihubiri amani kwa staili yake, pale alipoeleza kuwa baadhi ya vyombo vya habari vinaandika habari za uongo na uzushi.

Lusekelo alisema tabia hiyo inachangia kuondoa amani katika jamii na kama yeye angekuwa mtawala, angeminya uhuru wa habari. Katika ibada hiyo Lusekelo ambaye hivi karibuni alisema waandishi wa habari walioandika habari za kumchafua watakufa kabla ya Machi 2017 na baadaye kuwataka wamwombe radhi ili awasamehe, alisema angekuwa mtawala angehakikisha anavibana vyombo vya habari vinavyotoa habari za uchochezi.

Huku akitumia neno ‘uhuru wa kipumbavu’, alisema katika mitandao ya kijamii watu wenye imani mbalimbali wamekuwa wakitumia lugha ya kibaguzi jambo alilodai kuwa linatengeneza matabaka kwa waumini wa dini mbalimbali.

“Kuna watu wanalalamika makanisa yamekuwa mengi lakini wanashindwa kulalamika kama baa zimekuwa nyingi mtaani, ukienda Sinza huwezi hata kupiga hatua mbili utakuta baa,” alisema.

Alisema ikifika Juni mwakani waumini wa kanisa hilo watapata neema na baraka ya aina yake, huku akiwashukia maadui zake kuwa mpaka kufikia kipindi hicho watakuwa kimya.

Rais Magufuli na amani

Rais Magufuli ambaye alishiriki ibada ya Krismasi jana katika Kanisa Kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu mjini Singida, aliwataka wananchi kuendeleza amani na upendo na kuacha vitendo vya kubaguana kwa misingi ya dini, kabila, itikadi na kanda zao.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa misa hiyo iliyoongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Singida, Edward Mapunda Rais Magufuli alisema, “Watanzania wanatakiwa kuongeza juhudi katika kuchapa kazi kama alivyofanya Bwana Yesu.”

Alisema maeneo mengi nchini yanaonekana kukabiliwa na uhaba wa mvua na hivyo akawataka wananchi kutumia mvua chache zinazoendelea kunyesha kuzalisha mazao yanayokomaa haraka ili kuepuka upungufu wa chakula.

Rais aliwasisitiza wakazi wa mkoa wa Singida kunakolimwa alizeti kuchangamkia fursa ya ujenzi wa viwanda ili kuzalisha mafuta ya kupikia kwa wingi kwa kutumia zao hilo.

Imeandikwa na Celina Mathew, Charles James, Mary Mtuka na Jemah Makamba
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo