Serikali yamtibu aliyechora Ngao ya Taifa



Mary Mtuka

Nembo ya Taifa
SERIKALI imeahidi kumpa matibabu mmoja kati ya wachoraji wa Ngao ya Taifa, Francis Ngosha na kumpa makazi ya kudumu.

Hatua hiyo imekuja baada ya kusambaa picha kwenye mitandao ya kijamii zikimwonesha Ngosha akiwa na hali mbaya Buguruni, Dar es Salaam, alikokutwa akiishi kwenye chumba kimoja alichopewa na msamaria mwema.

Akizungumza Dar es Salaam jana kwenye hospitali ya Rufaa ya Amana, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangalah alisema mchango wa mzee huyo ni mkubwa na unathaminiwa na Serikali, hivyo ina jukumu la kuhakikisha anakuwa na afya bora.

"Kutokana na hali yake, tumeona kwanza tushughulike na matibabu kwa sababu ndilo la muhimu na baada ya hapo tutamtafutia makazi na kama atakubali atapelekwa katika kambi ya wazee wasiojiweza ya Nunge au tumtafutie nyumba,"  alisema.

Alisema Mzee huyo alitumia kipaji chake cha uchoraji jambo ambalo litadumu katika vizazi vyote vijavyo, hivyo Serikali ilimwagiza kuchukua hatua za haraka za kumsaidia.

Mkuu wa Kitengo cha Dharura cha Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Juma Mfinanga alisema wamepokea taarifa hiyo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu, ili kushughulikia kama ana tatizo la kiafya.

"Kwa mujibu wa wauguzi waliompokea juzi na taarifa iliyopo ameonekana na uchovu hivyo ingawa tayari walishaanza uchunguzi hivyo tutafanya uchunguzi zaidi ili kujua ni tatizo gani linamsumbua," alisema.

Mzee Ngosha alisema anaishi mwenyewe na mara nyingi husaidiwa na majirani. Ngosha alizaliwa mwaka 1931 na hakubahatika kupata watoto.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo