Waziri ataka barabara Tanroads ziwekwe lami


Stella Kessy

Edwin Ngonyani
NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani, ameutaka uongozi wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoani Morogoro kuhakikisha wanafanya matengenezo katika barabara zao ili zipitike katika kipindi chote cha mwaka.

Ngonyani alisema jana katika taarifa yake kuwa hilo limeanza kutekelezwa katika barabara ya Ifakara, Taweta hadi Madeke yenye urefu wa km 225) na barabara ya Ifakara kwenda Kihansi ya km 130 ambako upembuzi yakinifu umeshafanyika.

"Katika miaka hii mitano tutahakikisha maandalizi ya awali ya kuwezesha barabara hii kujengwa kwa kiwango cha lami yanakamilika na hivyo kutuwezesha kutenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi rasmi," alisema.

Alisema kuwa barabara hiyo ni kiungo muhimu kwa wakazi wa Ifakara na Kilombero kwa kuunganisha na mkoa wa Njombe na hivyo kukamilika kwake zitafungua fursa za kiuchumi na kibiashara kwa wananchi hao.

Ngonyani amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kutekeleza ahadi zote zilizotolewa kwa wananchi kwa kuunganisha mikoa mbalimbali kwa ujenzi wa barabara bora za viwango vya lami ili kurahisisha usafiri na kuongeza kasi ya maendeleo kwa wananchi.

"Serikali ya awamu ya tano ipo madarakani kwa ajili ya wananchi bila kujali itikadi zao, tumewaahidi kuwaletea maendeleo hivyo tutajenga barabara zote tulizoahidi kwa wakati ili wananchi waendelee kunufaika na matunda ya serikali yao,” alisema.

Aliongeza kuwa Serikali kupitia wizara yake itaboresha huduma za mawasiliano katika sehemu mbalimbali za nchi ili kuwawezesha wananchi kuwasiliana wakati wowote ili kukuza mahusiano yao kiuchumi, kibiashara na hivyo kukuza pato lao na la taifa.

"Tumeuomba uongozi wa kila wilaya utuletee maeneo ambayo huduma za mawasiliano hazijafika au zinasumbua ili sisi tuweze kuzishughulikia na kuzipatia huduma bora za mawasiliano,” alisisitiza.

Wakati huo huo, Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Suzani Kiwanga ameishukuru serikali kwa uamuzi wa kuiweka barabara hiyo katika mpango wa kuijenga kwa kiwango cha lami kwa kuwa itafungua fursa mbalimbali kwa wananchi ambao wataweza kusafirisha mazao yao kwenda katika sokoni kwa urahisi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo