Baregu amnasihi Polepole kuhusu Katiba

Celina Mathew

Humphrey Polepole
MJUMBE wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu, amemshauri Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole kupeleka mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwenye ngazi za juu za chama huku Mwenyekiti wake, Jaji mstaafu Joseph Warioba akisema hana la kusema.

Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya Polepole kueleza kuwa licha ya kukubali madaraka ya usemaji wa chama hicho, msimamo wake kisera wa Muungano wa Serikali Tatu unaopingana na matakwa ya chama hicho ambao ni wa Serikali Mbili uko palepale.

Akizungumza na JAMBO LEO jana, Profesa Baregu alisema ipo haja kwa Polepole kutumia fursa aliyopata kuishawishi CCM na kuieleza kiundani kuwa mapendekezo ya Tume yalikuwa na maana kubwa, hivyo kama anataka Muungano uendelee na uwe wa hiari na huru, mapendekezo yaliyopendekezwa yalikuwa na misingi hiyo.

"Hivyo anayosema Polepole, atusaidie ayachukue kuyapeleka hadi kwenye uongozi wa chama wa ngazi za juu, awaeleze wayaelewe ili mchakato wa Katiba mpya umalizike ukiwa na maoni ya wananchi," alisema.

Alisema mapendekezo ya Katiba ya Bunge Maalumu hayana maana yoyote kupigiwa kura ya ndio au hapana, kwa kuwa yalishatoka na hivyo kinachotakiwa ni maoni yaliyotolewa na wananchi wenyewe, kwa  kufuata Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwenye Rasimu ya Jaji Warioba.

"Kuna watu hawaamini kama mapendekezo yalitokana na wananchi, hivyo inabidi watambue kuwa lengo la Tume si kuvunja Muungano bali kuuboresha na kuuimarisha," alisema Profesa Baregu.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku ambaye alikuwa mjumbe wa Tume hiyo, alisema anachofanya Polepole kwa sasa, basi kinachosubiriwa ni Katiba kupigiwa kura na tangu wakubaliane kuhusu suala hilo, hakuna aliyekiuka maagizo.  

Chadema

Mkurugenzi wa Itikadi, Itifaki, Uenezi, Mawasiliano na Mambo ya Nje, Chadema John Mrema alimpa pole Polepole kwa kupewa kazi ya kukisemea chama ambacho hakubaliani na misimamo yake kisera, huku akitolea mfano suala la Katiba Mpya hasa ikizingatiwa kuwa moja ya misimamo yake ni serikali tatu kinyume na msimamo wa CCM ambao ni wa serikali mbili.

Mrema alisema Polepole amepewa kazi ya kukisemea chama ambacho hakijui, kwani hana rekodi ya kukulia ndani ya UVCCM au kuwa na nafasi yoyote zaidi ya hivi karibuni kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya, hivyo amekubali kukisemea chama ambacho hakijui, “hivyo atasema nini?

Akizungumzia mabadiliko ya ratiba za vikao vya ndani ya CCM alisema ni dalili za wazi kuwa wamepoteza mvuto na hawana ajenda za kujadili, hivyo kuamua kuongeza muda wa vikao ili wapunguze kuhojiwa kwa Serikali yao ambayo hadi sasa imesababisha maisha kuwa magumu zaidi kwa Watanzania, hata wanachama wao wanaisoma namba.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Benson Bana alisema alichosema Polepole ni kuwa kwenye utendaji wake atakubaliana na kitakachoamuliwa na chama hicho kwenye vikao na mikutano ingawa msimamo wake utabaki palepale.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo