Mabadiliko CCM fursa upinzani


Waandishi Wetu

WAKATI Chama cha Mapinduzi (CCM) kikifanya mabadiliko ya mfumo wake wa uongozi, ikiwa ni pamoja  na kuondoa baadhi ya nafasi na kupunguza idadi ya vikao, vyama vya upinzani nchini vimesema hayawezi kuwayumbisha wala kukwamisha harakati zao za kutaka kushika dola.

Huku wakijigamba kuwa wamekuwa wakiibuka na ushindi katika chaguzi mbalimbali lakini ushindi huo unaporwa na CCM, walisema pamoja na mabadiliko hayo, chama hicho tawala ni kile kile kilichobadilika ni muundo tu.

Hivi karibuni chama hicho kilifanya mabadiliko yanayolenga kubana matumizi na kuongeza ufanisi, huku baadhi ya watu wakipitiwa na panga hilo la mabadiliko, wakiwemo makatibu wasaidizi wa mikoa 32 na wilaya 139 sambamba na kupunguzwa kwa wajumbe 230 wa Halmashauri Kuu kutoka 288 hadi 158, wajumbe 10 wa Kamati Kuu kutoka 34 hadi 24.

Fagio hilo pia limewaondoa wajumbe watatu wa kamati ya siasa ya mkoa, huku ikipunguza wajumbe wanne katika Kamati ya Siasa ya Wilaya sambamba na kufyeka vyeo ambavyo havijatamkwa kwenye Katiba ya chama hicho.

Mtazamo wa wapinzani

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, John Mnyika alisema, “CCM ni ile ile na uongozi wake ni uleule. Mabadiliko hayo madogo waliyoyafanya hayawezi kuzuia haja na hoja za mabadiliko.”

Mbunge huyo wa Kibamba alisema wananchi wanahitaji mabadiliko makubwa kupitia Ukawa, huku akibainisha kuwa kama CCM ingekuwa imejipanga, Rais John Magufuli angeruhusu kufanyika kwa mikutano ya hadhara, kama ilivyokuwa awali.

“Ukawa tunachopaswa kufanya sasa ni kuwaongoza wananchi kudai Tume huru ya uchaguzi ili iwe rahisi kuwashinda CCM mwaka 2020,” alisema Mnyika na kuongeza;

“Kwa sasa tumewabaini mbinu na hujuma zao kwa hiyo tumejipanga mapema. Kupitia mikutano hii ya ndani waliyoiruhusu, tutajipanga kupambana nao.”

Katibu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Juju Danda alisema mabadiliko ya CCM hayawezi kuwa na tija katika vyama vya upinzani iwapo Katiba haitakuwa inafuatwa.

Alisema kwa muda mrefu kumekuwepo maamuzi ya mtu mmoja katika kila jambo, hivyo hata kama wangekuwa wana CCM wawili wanaweza kuwa kero au raha kwa wapinzani iwapo watafuata Katiba.

“Hapa hatuzungumzii mabadiliko yao kuwa ya wengi au wachache, ila tunataka Katiba ifuatwe na kila mmoja wetu kwa sababu ndio inatuongoza, si mtu kuamua hakuna mikutano halafu afuatwe,” alisema.

Alisema kitendo cha mwenyekiti wa CCM, John Magufuli kupunguza idadi ya wajumbe si kwamba anakipenda chama au Serikali ila msingi wake ni kujitawalisha madaraka na kusababisha wanachama wamuogope.

Mwenyekiti wa Chama Cha Kijamii (CCK), Constatine Akitanda alisema mabadiliko ya CCM hayawezi kuleta mabadiliko, huku akisisitiza kuwa usawa utapatikana iwapo kutakuwa na uwanja huru wa kufanya siasa.

“Siasa sawa inategemeana na ngoma ambayo itapigwa ambapo ni uwanja sawa. Sasa kwa hapa nchini hakuna uwanja sawa hivyo ni ngumu kusema kuna fursa kwetu,” alisema.

Alisema CCM na Serikali wanapaswa kutambua kuwa siasa ni maisha ya watu hivyo inapaswa kuheshimu na kutoa ushirikiano baina yetu.

Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma), alisema haamini katika mabadiliko hayo na kuwataka wateule kusimamia misingi ya haki na kuwa wavumilivu, kwani siasa ni mchezo wa uvumilivu zaidi.

Rungwe alisema CCM imekuwa katika wakati mgumu kwa kipindi cha hivi karibuni, ila kupitia mabadiliko hayo inaweza kupotea zaidi na kuwa wanachopoteza kwa sasa ni kufanya ubadhirifu katika halmashauri.

“Kimsingi sisi tunafanya kazi kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa namba 5, lakini kikwazo kikubwa ni kutofuatwa kwa Katiba,” alisema.

Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa alisema kiujumla wateule wapya si tishio kwa siasa za Tanzania, ila alitoa angalizo kwa kutaka wapewe muda zaidi ili waweze kupimwa.

“Tuwape muda hawa ndio wapiya pamoja na ukweli kuwa si watu wa kutisha,” alisema.

Mwenyekiti wa ADC, Hamad Rashi Mohamed alisema mabadiliko hayo ya CCM ni ya kupongezwa na kuwa vyama vya upinzani vinapaswa kuiga njia hiyo.

Alisema hakuna haja ya kuangalia mabadiliko hayo kwa misingi ya kukabiliana na wapinzani ila ni vema vyama vya upinzani na viongozi wake kujifunza zaidi njia ya kufanya kazi kwa kujitathmini zaidi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo