Kauli tano za JPM zilizotikisa 2016


Waandishi Wetu

WAKATI mwaka 2016 ukielekea ukingoni, hotuba tano zilizotolewa na Rais John Magufuli zimetajwa kuwa ndizo zilizotikisa zikitoa mwelekeo wa uongozi wake, Taifa na changamoto, huku wachambuzi mbalimbali nchini wakizichambua na kueleza watarajio yao kwa mwaka ujao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na JAMBO LEO, wachambuzi hao wamesema katika hotuba hizo ameweza kuonesha mweleko mzuri katika masuala mbalimbali yaliyoonekana kutaka kuitikisa nchi yakiwemo; ubadhilifu, uwajibikaji, rushwa, ufisadi, elimu, watumishi hewa na uchumi.

Tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano Novemba 5 mwaka jana, Dk Magufuli amesafiri nje ya nchi mara mbili tu, muda mwingi akiutumia ‘kuweka nchi sawa’, huku mara kadhaa akinukuliwa akisema mtangulizi wake, Jakaya Kikwete amemwachia kazi ngumu kutokana na nchi kuwa ya wapiga dili kila kona.

Hotuba hizo tano ni ile aliyoitoa wakati wa uzinduzi wa ndege mbili za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), ufunguzi wa mkutano wa wahandisi, alipokabidhiwa uwenyekiti wa CCM, kuapishwa kwa makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu Ikulu na alipozungumza na wana CCM kwa mara ya kwanza baada ya Uchaguzi Mkuu.

“Amekuwa muwazi katika vita dhidi ya kupambana na rushwa na ufisadi. Wakati wa kampeni aliahidi kuanzisha Mahakama ya Mafisadi na kweli ameanzisha, jambo ambalo limejenga imani kubwa kwa wananchi,” alisema George Kahangwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanataaluma Chuo Kikuu Dar es Salaam (Udassa).

“Alisistiza kuhusu uwajibikaji na sasa tunauona mafanikio. Hapo ndipo ulipoanza ule msemo wa ‘kutumbua majipu’ lengo likiwa kuhakikisha wazembe wanakaa kando na wanaobaki wanafanya kazi ipasavyo na kuachana na mazoea.”

Dk Kahangwa alisema kiongozi mkuu huyo wa nchi pia amejitahidi kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya viwanda, ikiwa ni pamoja na kuvifufua vilivyokufa sambamba na kukaribisha wawekezaji huku akitea mfano wa mvutano ulioibuka hivi karibuni kati ya Serikali na kiwanda cha saruji cha Dangote.

Hamad Salim wa Chuo Kikuu Huria (OUT), aliungana na Dk Kahangwa kuhusu mahakama ya mafisadi, kusisitiza kuwa ni jambo ambalo halikutarajiwa kuwepo nchini.

“Yapo mambo ambayo ameweka njia ingawa yanaweza kuwa na changamoto zake. Mfano ni elimu bure bado kuna changamoto kadhaa sambamba na uanzishwaji wa viwanda,” alisema.

Alisema mkakati wa Serikali kuhakiki vyeti vya watumishi wake umefungua njia ya kudhibiti mapato na matumizi kutokana na kuwepo kwa kundi kubwa la wafanyakazi hewa waliokuwa wakikwamisha kupatikana kwa fedha kwa ajili ya maendeleo.

“Ameweka msingi mzuri katika baadhi ya mambo kama elimu bure, uwajibikaji na uchumi wa viwanda ingawa bado matunda hayajaonekana. Nadhani anakwama kwa sababu ya kukosekana kwa sera maalum kwa ajili ya kuzinyanyua sekta za viwanda, elimu na hata kupambana na mafisadi,” alisema Profesa Gaudence Mpangala, Mhadhiri mwandamizi Chuo Kikuu Ruaha.

Wakati Profesa Mpangala akisema Rais Magufuli amekuwa akitoa matamko mengi na kudai ni tofauti na ufanisi wa Serikali yake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema ameweka msingi mzuri katika Serikali yake, hasa kurejesha uwajibikaji na nidhamu kwa watumishi wa umma.

“Katika mwaka wake wa kwanza wa uongozi amerejesha uwajibikaji na nidhamu jambo ambalo limejeresha hali ya kufanya kazi ukichangiwa zaidi na utumbuaji wa majipu,” alisema Dk Bana.

Huku akipongeza kuanzishwa kwa mahakama ya mafisadi Dk Bana alisema, “ Mwaka ujao sitarajii kuona utumbuaji majipu kwa sababu ameshajenga msingi mzuri katika kila nyanja. Anachopaswa kufanya ni kuongeza wigo wa upatikanaji wa ajira na kuwafanya Watanzania kuwa wazalishaji badala ya kuendelea kuwa wachuuzi.”

Hotuba tano

Agosti 12 mwaka huu, mwezi mmoja baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli aliwataka wanachama na viongozi wa chama hicho tawala kumvumilia kwa maelezo kuwa anataka kurejesha heshima, imani na maadili yaliyopotea ndani ya chama hicho

“Mahali nitakapoamua kunyosha nitanyooshea hapo hapo.

Inawezekana ujio wangu ndani ya CCM usiwafurahishe baadhi ya watu lakini nina uhakika wanachama wetu zaidi ya milioni nane watafurahi. Nimeamua kufanya kazi kwa uwazi ili kila pato la chama lionekane,” alisema

Katika hafla fupi ya kumpokea iliyofanyika ofisi ndogo za chama hicho zilizopo mtaa wa Lumumba, Rais alihoji zinapokwenda fedha za viwanja 410 vya CCM, Fedha za Sukita sambamba na za jengo la umoja wa vijana wa chama hicho (UVCCM), jumuiya ya wazazi, viwnaja vya mpira na umoja wa wanawake (UWT).

Kiapo Ikulu

Machi 7 mwaka huu katika hafla fupi ya  kuapishwa kwa makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu 26 iliyofanyika  Ikulu ilikuwa ya aina yake kutokana na kuapa mara mbili, huku Rais Magufuli akiwaeleza kuwa asiyeweza kazi “aseme na asile kiapo, akae kando”.

“Inawezekana tulizungumza kwa ujumla lakini kumbe si wote wanakubali masharti kuhusu rushwa, kutoa vitu vya upendeleo. Kwa hiyo niwaombe makatibu wakuu pamoja na kwamba mlishaapa kwangu, ambaye hakubaliani na hilo asimame kando ili waliobaki waendelee,” alisema Rais Magufuli kabla ya kiapo hicho.

Licha ya kauli hiyo, hakuna ahata mmoja aliyepinga kiapo hicho.

Kuhamia Dodoma

Julai 24 mwaka huu baada ya kuchaguliwa kuw amwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli alitangaza ahadi kwa wanachama hao, kuwa amebakiza miezi minne na miaka minne kabla ya kumaliza kipindi chake cha miaka mitano na kusema kabla ya kumaliza kipindi hicho, atakuwa amehamishia serikali yote Dodoma.

Magufuli alisema kwa sasa miundombinu ya Dodoma inawezesha serikali kuhamia huko, kwa kuwa barabara za kutoka Makao Makuu hayo ya serikali kwenda sehemu mbalimbali nchini, zinapitika kwa lami.

Mbali na barabara, alisema pia huduma kwa ajili ya maisha ya watu nazo zinapatikana kwa kuwa mkoa huo una uzoefu wa kuhudumia wabunge, wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM na mikutano mingine, huku mkoa huo ukiwa na Chuo Kikuu cha Dodoma, ambacho ndio kikubwa kuliko vyote nchini.

Uzinduzi ndege ATCL

Septemba 28 mwaka huu wakati wa uzinduzi wa ndege mbili aina ya Bombardier Dash 8 Q400, Rais Magufuli aliwabeza walioziponda ndege hizo kuwa hazina kasi  huku akieleza sababu za kununuliwa kwake kwa fedha taslimu badala kulipa kidogokidogo.

Katika uzinduzi huo, aliomba  bodi na menejimenti ya ATCL kutoruhusu kiongozi wa serikali kusafiri bure hata kama ni yeye au waziri wa Wizara ya Uchukuzi au bodi kwani kuna wakati wanakuwa wanajipendekeza wakati wanatakiwa kufanya biashara.

Mkutano wa wahandisi

Septemba Mosi mwaka huu wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mkuu wa 14 wa wahandisi, Rais Magufuli aliweka wazi mkakati wake wa  kuwadhibiti watu wanaodaiwa kuficha fedha katika majumba yao, akiwataka kuziachia ziingie kwenye mzunguko kwa maelezo kuwa anaweza kuamua kubadili fedha ili zinazofichwa na watu hao wakose mahali pa kuzipeleka.

Alisema watu hao wamekuwa na utaratibu wa kutoa fedha zao katika mabenki na kuzificha kwa kuogopa kuwa atabaini kiasi walichonacho, kuwataka kuachana na tabia hiyo kwa sababu fedha hizo ni zao.

“Na wajiandae naweza kuamua baada ya siku mbili tatu nabadilisha fedha  na hizo zilizofichwa katika magodoro ziozee huko…, ni nafuu mzitoe  mziweke katika mzunguko zikafanye kazi.”
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo