JPM aapisha viongozi wapya


Mwandishi Wetu

RAIS John Magufuli, amewaapisha viongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na majaji wa Mahakama ya Rufani aliowateua juzi.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari, ilieleza kuwa hafla ya kuwaapisha viongozi hao, ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali.

Miongoni mwa viongozi hao ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Anjellah Kairuki, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju na viongozi wengine.

Walioapishwa ni Jaji Semistocles Kaijage kuwa Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Hamid Mahmoud Hamid, kuwa Makamu Mwenyekiti wa NEC na Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Harold Nsekela kuwa Kamishna wa Maadili katika Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Viongozi hao watashika nyadhifa hizo kwa miaka mitano.

Majaji walioapishwa kwa ajili ya Mahakama ya Rufani, ni Jaji Rehema Mkuye; Jaji Sivangilwa Mwangesi, Jaji Gerald Ndika na Jaji Jackobs Mwambegele.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uturuki nchini, Yesamin Eralp ambapo viongozi hao walizungumzia uhusiano kati ya Tanzania na Uturuki, hususan katika masuala ya ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo.

Aidha, Rais Magufuli na mkewe Mama Janeth, walimtembelea na kumpa pole Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kumpa pole ya kifo cha dada yake Efrazia Pengo (79), aliyefariki dunia juzi katika kijiji cha Mwazye, wilaya ya Sumbawanga, Rukwa.

Rais Magufuli na Mama Janeth walimtembelea Kardinali Pengo katika makazi yake Kurasini, Dar es Salaam.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo